VIVUMISHI

      No Comments on VIVUMISHI

VIVUMISHI 

Kivumishi ni neno au fungu la maneno linaloeleza zaidi juu ya nomino. Kivumishi ‘huvumisha’, yaani hueleza mtu namna alivyo au kitu nama kilivyo, kinavyofikirika au kufikiriwa. Pia huonyesha idadi fulani ya kile kinachozungumziwa. Kuvumisha ni kutoa habari.

Tunaweza pia tukasema, vivumishi ni maneno yanayosifu au kufasili sura za nomino.

AINA ZA VIVUMISHI 

1. VIVUMISHI VYA SIFA: Haya ni maneno yanayotaja sifa au tabia ya nomino inayovumishwa. Kwa mfano,  Mtoto mzuri amefaulu mtihani.

2. VIVUMISHI VYA IDADI: Hivi ni vivumishi vinavyoonyesha idadi ya nomino zinazozungumziwa. Vivumishi hivi huweza kuwa:

  • Vya idadi mahsusi/maalum  (idadi dhahiri). Kwa mfano, wanafunzi wawili walishiriki mashindano ya uandishi wa insha.
  • Vya idadi ya jumla(idadi isiyodhahiri). Kwa mfano, watu wengi walihudhuria harusi hiyo.

3.VIVUMISHI VIONYESHI (VIASHIRIA): Vivumishi vinavyotumika kuonyesha mahali kitu kilipo kwa njia ya kuashiria. Kwa mfano, Gari lile liliegeshwa karibu na duka kuu.

4. VIVUMISHI VIULIZI: Vivumishi vinavyodhihirisha kuwepo kwa swali. Hutumiwa ili kuuliza swali kuhusu nomino. Kwa mfano, Rahma amejifungua mtoto gani?

5. VIVUMISHI VIMILIKISHI: Vivumishi hivi huelezea ni nani anayemiliki nomino. Kwa mfano, Kikombe changu ni kidogo.

6. VIVUMISHI VYA MAJINA: Hizi ni nomino ambazo hutumika kama vivumishi. Hutumika ili kuelezea zaidi maana ya majina mengine. Vivumishi hivi vikiwa peke yake huwa ni majina tu, lakini vikiunganishwa na majina mengine hufanya kazi ya wasifu (yaani kusifu) au kuelezea jina linalotangulia. Kwa mfano,  Mwanamke tajiri amekuja shuleni.

Tajiri ni nomino iwapo itatumika bila neno mwanamke. Kwa mfano, tajiri amekuja shuleni.

7. VIVUMISHI VYA PEKEE: Hivi hutokana na mizizi ‘-ote, -o-ote, -ingine,  -enye na -enyewe’. Kwa mfano,  Wanafunzi wengine wamefika shuleni.

8. VIVUMISHI VYA A-UNGANIFU: Hivi ni vivumishi vinavyoundwa kwa a-unganifu na hutumika kutoa sifa za nomino. Kwa mfano, daftari la mwalimu lipo juu ya meza.

9. VIVUMISHI VYA KUREJESHA (VIREJESHI): Hivi ni vivumishi vinavyotumika kurejelea nomino. Hujengwa kwa kutumia ‘O-rejeshi’. Kwa mfano,  mtoto huyo alikunywa uji wa wimbi.

10. VIVUMISHI VYA KUSISITIZA(VISISITIZI): Hivi hutumika kusisitiza nomino iliyotajwa hapo awali. Kwa mfano,  Daftari lili hili ndilo alilotumia.

MAREJELEO

  1. Kimani Njogu na Dorothy K. Nganje, kiswahili kwa vyuo vya ualimu: Jomo Kenyatta Foundation 2006.
  2. Kimani Njogu, Alice Mwihaki na Aswani Buliba, Sarufi ya kiswahili: uchanganuzi na matumizi: Jomo Kenyatta Foundation 2006.
  3.  G. Waihiga na K.W. Wamitila, chemichemi za kiswahili kidato cha pili 2003

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *