KIPI CHA AWALI? YAI AU KUKU?

      No Comments on KIPI CHA AWALI? YAI AU KUKU?

MAIYA
Natoa kitendawili, malenga nipulikani
Nawauliza suali, munipe jibu yakini
Likae kwenye akili, kilipima na mizani
Ni kipi kitu awali, baina kuku na yai

FARWAT
Kigumu Kitendawili , ila nitajitahidi
Umeniweza kwa kweli, mwisho nataka zawadi 😅
Naifungua akili, lisilobudi hubidi
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Kweli nataka kujuwa, jambo hili kiundani
Niweze kulielewa, litue mwangu moyoni
Na sababu za kumwaya, uniishe ushindani
Kipi kilotangulia, baina kuku na yai

FARWAT
Fungua akili dada, nayo macho kadhalika
Leo nakupa faida, uelewe bila shaka
Maelezo ya ziada, nitakupa ukitaka
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Kila nikitafakari, ninalikosa jawabu
Sana ninajishauri, lakini sipati jibu
Na aje alo hodari, wa maneno kukutubu
Anijuze hii siri,ni kuku au ni yai?

FARWAT
Usifikirie sana, ukapasuka akili
Jawabu liko bayana, kulihusu lako swali
Kuku unavyomuona, yeye ndiye wa awali
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Kuku ninaowaona, kila ninakopitia
Ni wote wametokana, na yai ninavyojua
Na yai yajulikana, kuku ndo wanatoa
Nipe jawabu la kina, ni kuku au ni yai?

FARWAT
Kuku unaowaona, ndio wataga mayai
Wakatoka wao wana, wakaupata uhai
Kuku akikosekana, litapatikana yai?
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

FARWAT
Bado hujaniridhisha, kuutuza moyo wangu
Sana wanibabaisha, katika akili yangu
Naomba nielewesha, nikufahamu mwenzangu
Vipi kuku kuhuisha, bila yai ndugu yangu

FARWAT
Nisikilize swahibu, tena uwe na makini
Kwa hakika ‘takujibu, ukuishe ushindani
Nitakupa na sababu, uelewe kwa yakini
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Ushanikoroga sana, nimepoteza ramani
Sio kuwa nashindana, halingii akilini
Yai lilitoa mwana, ndo kataga duniani
Iweje leo wanena, yai ndilo la thineni

FARWAT
Wajikoroga naona, ndugu yangu taratibu
Mayai yametokana, kwenye kuku ndiyo jibu
Hilo linaonekana, lipo wazi ya swahibu
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Niongezee dalili, linawezekana vipi
Zitue kwenye akili, nijue nishike lipi
Nitambue ilo kweli, kilichoanza ni kipi
Kama yai ni la pili, nae kuku katokapi?

FARWAT
‘Meumbwa kuku sikia, na Mungu mola mwenyezi
Mungu ametuumbia, kama ‘livyoumba mbuzi
Kisha yai katokea, kataga kuku mzazi
Yai ni kitu cha pili, naye kuku wa wahedi

MAIYA
Sasa nimekufahamu, metoa taka sikio
Umenituliza hamu, u makini wangu moyo
Kumbe cha kwanza muhimu, Mola ndiye aumbao?
Jawabu liko timamu, na zawadi yako hiyo🐓

FARWAT
Ni vizuri ndugu yangu, kuwa umenielewa
‘Metua mtima wangu, kwamba sasa umejuwa
Shukurani nyingi zangu, kwa zawadi ‘lo muruwa
Kweli yai ni la pili, naye kuku wa wahedi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *