MAWAIDHA YA BABU

      No Comments on MAWAIDHA YA BABU

MWANA
Shikamoo wangu babu
Kukusalimu wajibu
‘Metuamuru wahabu
Heshima kuwapatia

BABU
Marahaba ya kijana
Habari za tangu jana
‘mefurahi kukuona
Kwako mi najivunia

MWANA
Za tangu  Jana ni njema
Nami pia ni mzima
Sina panaponiuma
Namshukuru jalia

BABU
‘Mefurahi kusikia
Kuna mambo ainia
Nataka kukuambia
Nakusihi zingatia

MWANA
Mimi nimemakinika
Tayari kunufaika
Busara yako hakika
Mimi naiaminia

BABU
Kwanza jambo lilo aula
Muogope wako mola
Usiziache zote swala
Madhambini kajitia

Shikilia sana dini
Iwe thabiti imani
‘kiondoka duniani
Pema upate shukia

Pili hao marafiki
Wengine ni wanafiki
Wakifanya ufasiki
Siwaandame sikia

Na wengine ni wahuni
‘Takutia hasarani
Wakushushe na thamani
Mwishoni ukajutia

Kwa hiyo jiweke mbali
Uyafanye ya halali
Umridhishe jalali
Na wazazi wako pia

Rafiki wa kufuata
Ni yule aso matata
Vitabu huvikamata
Na bidii akatia

Na pia hiyo adabu
Ishikilie shababu
Utaziepuka tabu
Maisha’tafurahia

Nisikilize ghulamu
Wazazi kuwaheshimu
Hilo ni jambo muhimu
Mola kalihimizia

Roho yako iwe Safi
Na laini kama sufi
Mama ‘simwambie uffi
Radhi akakukatia

Na ndugu zako wapende
Usijifanye afande
Kuwapiga kwa makonde
Chuki ukajijengea

Kiunge sana kizazi
Uyajenge na mapenzi
Watu wako uwaenzi
Ni muhimu familia

Haya ukiyafuata
Kweli utametameta
Utangara kama nyota
Katika hini dunia

MWANA
Nimekusikia babu
Hekima yako ajabu
Wala sioni sababu
Maneno kupuuzia

Tafuata hima hima
Yote ulioyasema
Nitashika yalo mema
Maovu Kuyakimbia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *