KUPE KAMGANDA N’GOMBE

      2 Comments on KUPE KAMGANDA N’GOMBE

Nikupe kisa swahibu, kilichomfika n’gombe
Yalimkuta masaibu, kikamkata kijembe
Alitafuta majibu, asipate hata chembe
Kupe kamganda ngombe, hakujali zake pembe

Mwenyeji kangia kati, ngombewe kumnusuru
Kwa mno kajizatiti, ili aipate nuru
Karushiwa kibiriti, akapiga kubwa nduru
Kupe kamganda ngombe, hakujali zake pembe

Kupe kainyonya damu, ni nyingi sio kidogo
Damu kaiona tamu, katu hakujali zogo
Kashikilia hatamu, miaka hadi miongo
Kupe kamganda ngombe, hakujali zake pembe

Mwenyeji kashika tama, hana tena yeye jinsi
Amebaki kulalama, maisha sio rahisi
Imepotea salama, kupe amekuwa nuksi
Kupe kamganda ngombe, hakujali zake pembe

Ngombe amedhoofika, hali yake taabani
Tamaa imekatika, mwenyeji hana amani
Kupe alomakinika, ameleta kisirani
Kupe kamganda ngombe, hakujali zake pembe

2 thoughts on “KUPE KAMGANDA N’GOMBE

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *