ELIMU HASI AU CHANYA?

      No Comments on ELIMU HASI AU CHANYA?

ELIMU HASI AU CHANYA?
Kaka
Hatari mno nasema, Mwana kufika chuoni
Ati aenda kusoma, Masomo ya uzunguni
Mwana hafai kusoma, Atakua majununi
Awe nyumbani na mama, Ajifunze tamaduni
Dada
Akhi unanishangaza,Kwa hayo maneno yako
Elimu ndiyo mwangaza, amri ya mola wako
Ni zote mbili sikiza, tegesha sikio lako
Basi ‘siwe tapuuza, ukapata hangaiko

Kaka
Kipi hasa mwatafuta, Nyie huko darasani
Ambacho hamkupata, Mlipotoka nyumbani
Hamuoni ni karata, Ya kutiwa utumwani
Wangu wasia we shika, Masomo si ya thamani

Dada
Tunatafuta elimu, tuupate ufunuzi
Ili pia tujikimu, tusiufanye upuzi
Na watu watuheshimu, na tungare kama mwezi
Tatubariki Rahimu, ya Rabbi Mola mlezi

Kaka
Nani alokuambia, Elimu itakukimu
Tena akakusifia, Ili uipate hamu
Mie sijaivamia, Na wala sijahitimu
Lakini najifanyia, Yakwangu ya kujikimu

Dada
Si kujikimu pekee, nduu yangu nisikia
Tena na yakuelee, haya ninayokwambia
Sio kazi tu pekee, elimu hukupatia
Na heshima ya kizee, ‘tapewa na jumuia

Kaka
Dadayangu huelewi, Haya ninokuambia
Unajitia uziwi, Na macho kuyafumbia
Elimu si ustawi, Wa maisha nisikia
Tena sio bora kawi, Yako kujisaidia
Dada
Sikubaliani nawe, abadani kataani
Umekuwa kama jiwe, hunielewi jamani
Kisikupate kiwewe, akakughuri shetani
Elimu unielewe, ni msingi maishani

Kaka
Babuyo kasoma wapi, Na nyanyayo kadhalika
Lishika mkondo upi, Uzeeni wakafika
Ama ni elimu ipi, Wanawao walishika
Hata ukinipa pipi, Elimu sitaiteka

Dada
Usilete ya zamani, tugange yanayokuja
Usilete ushindani, Kwa zilizo finyu hoja
Ya nyanya yahusiani, Usinisemeshe mja
Elimu ina thamani, Naishika yangu hoja

Kaka
Tajuaje uendako, Utokako kisahau
Ndipo hapo machafuko, Mnayaleta wadau
Tamaduni njema zako, Kiacha tasema lau
Dada acha michepuko, Elimu sio mdau

Kaka
Ajabu wanosumbua, Ati ni wale wasomi
Akili hazijakua, Kwa huo wao usomi
Jamii yawatambua, Wengi wanapenda ngumi
Masomo sio murua, Acheni wenu uvumi

Dada
Nawe sikubaliani, ninakupinga vikali
Waliofika shuleni, wanazo nyingi akili
Na ovyo hawapigani, ni watu walo aali
Wanaipenda amani, na pia wanaijali

Kaka
Wana wanaharibika, Mumo humo mashuleni
Mbovu tabia washika, Zisizo za tamaduni
Jamii yaporomoka, Kisa elimu jamani
Langu bado nimeshika, Elimu ni uhaini

Dada
Si wana wote elewa, ambao waharibika
Jinsi walivyolelewa, yachangia bila Shaka
Wapo wenye mwendo Sawa, tena chuo wamefika
Mwishowe wakaolewa, na tena wakasifika

Kaka
Mbona mnajisumbua, Mwajitesa vitabuni
Si kwamba nawaumbua, Nataka muwe makini
Masomo yatawaua, Ni maradhi ya moyoni
Ukitaka vyema kua, Siingie darasani

Dada
Situpotoshe kijana, hebu kuwa na hekima
Masomo yana maana, aso nayo ni kilema
Kwa hiyo ufanye hima, tuunge tunaosoma
Utafurahika Sana, na kuipata heshima

Kaka
Zako hoja mefahamu, Mwenzangu nisikia
Elimu jambo adhwimu, Muhimu kuisakia
Mjinga hana muhimu, Katika yetu dunia
Shuleni twende qaumu, Tuweze jisaidia

Wote
Mwisho hapa tumefika, Usia tunawapeni
Elimu jambo mwafaka, Hivyo jamii someni
Ni amri ya Rabuka, Iliyopo vitabuni
Tulotunga kwa hakika, Farwatha na Huseni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *