HAKUNA KAMA MAMA

      No Comments on HAKUNA KAMA MAMA

 

Naanza langu shairi,kwa mapozi na madaha
Nataka kuikariri, niliyonayo furaha
Nimepewa na qahari,nakwambia si mzaha
Furaha yenyewe gani? Ni kipenzi wangu mama.

Baada mola karima,na mtume hashimia
Wa kufuata ni mama,nadhani mwanisikia
hivyo tufanyeni hima,mazuri kumtendea
Hata wapande milima, hakuna kama we mama.

Niliyonayo mapenzi, nashindwa kuelezea
Moyo ungekuwa Nazi,basi ningeupasua
Ili kuyaeka wazi, yaliyo kwenye kifua
Uingereza uswazi, hakuna kama we mama.

Wewe Ni fahari yangu,mwanao najivunia
Huburudi moyo wangu,wewe kikufikiria
Huondoka shida zangu,wewe kikuelezea
Shariani takaungu, hakuna kama we mama.

Hujihisi mi mpweke,mamangu ukiwa mbali
Na natamani niruke,niweko pako mahali
Abadan nisiondoke,niipate mi sahali
Arusha hadi temeke, hakuna kama we mama.

Kikombe tele machozi,mimi hunimiminika
Wala sinayo simanzi,Ila ni kufurahika
Kukupata we kipenzi, mama yangu msifika
Lamu na hata kibwezi, hakuna kama we mama.

Hata ‘kijaza kurasa,au kizima kitabu
Maneno sitayakosa,kukusifu we muhibu
Au mbinu za kisasa,zote mi nitajaribu
Canada na ufaransa, hakuna kama we mama.

Cha kukulipa mi Sina,ewe wangu msifika
Ila ahadi nanena,Kuwa utafurahika
Wewe utapaka hina,kwa sana kupumzika
kule India hadi China, hakuna kama we mama.

Na bidii uendazo,ili kunifurahisha
Na kutilia mkazo, mwanao kunisomesha
Hayo yote si mchezo,taji mi nakuvalisha
Kampala kalisizo, hakuna kama we mama.

Penzi lingekuwa jani,Basi ningekupa mti
Au Lulu baharini,ningeisaka habibti
Ila kwa yako thamani,nakuombea jannati
Mashariki na kusini, hakuna kama we mama.

Nakuombea mannani,upate umri twawili
Akhera na duniani,uishi kwa njema hali
Na pia kule peponi,uwe na wetu rasuli
Magharibi kaskazini, hakuna kama we mama.

Hapa mwisho nakomea,yanatosha hayo Sasa
Lau nitaendelea,nitazijaza kurasa
Hakika nimetembea,mabara hata Mombasa
Ila sijajionea, mfano kama we mama.

Kama ilivyo desturi,kikomoni nikifika
Mwisho wa langu shairi,jina langu hutamka
Basi ninalikariri,Ni farwatha farshika
Tanga pia Zanzibari, hakuna kama we mama

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *