Naanza hapa kunadi, umati kuwausia
Namshukuru wadudi, kunipa njema afia
Mada leo ni hasadi, mno tunojitakia
Sio kwa kila neema, tutangaze hadharani
Mwana umejaaliwa, bila shaka ni neema
Kweli umebarikiwa, Leo unaitwa mama
Ila si jambo la Sawa, kuposti bila kukoma
Sio Kwa kila neema, tutangaze hadharani
Kakujaalia manani, bidii nayo akili
‘mefaulu mtihani, watuma kila mahali
Jamani tuwe makini, hasadi ikae mbali
Sio Kwa kila neema, tutangaze hadharani
Amekuja kwenu mume, harusi tukaicheza
Mbio mithili umeme, wasapu wajitangaza
Na marafiki Kwa shime, pichazo wazisambaza
Sio Kwa kila neema, tutangaze hadharani
Leo umekula kuku, hatutopumua basi
Mapicha huku na huku, waposti tena kwa Kasi
Tuwache uzumbukuku, tutafakari insi
Sio kwa kila neema, tutangaze hadharani
Wapo wanaotamani, kuvipata vyako vyote
Kinyongo ndani Kwa ndani, wanavimezea mate
Ndugu tutahadharini, mabaya yasitukute
Sio kwa kila neema, tutangaze hadharani
Nawe umeshasikika, Hasadi jambo hatari
Usia umeshafika, Waja tutatahadhari
Pongezi zamiminika, Kwako wewe mshairi
Umati kuelimika, Bila Shaka hiyo kheri