MAMA

      1 Comment on MAMA

NAANZA  YANGU KAULI
SHUKURANI  KWA  JALALI
KWA  KUNIPA  USAHALI
SHAIRI  KUJITUNGIA

NITAMALIZA VITABU
KWA KUMSIFU MUHIBU
NA HATA NIKAJARIBU
SIFA SITOMALIZIA

KWA MAPENZI MOTO MOTO
ULINILEA MTOTO
MAJANGA NAYO MAZITO
YOTE UKAVUMILIA

TUMBONI TISA MIEZI
KUJITETEA SIWEZI
ILA KWA YAKO MAPENZI
NIPO NILIPOFIKIA

NILIPOKUWA MCHANGA
ULIYAPATA MAJANGA
KUKESHA MIDA YA WANGA
ILI NIACHE KULIA

KATIKA YAKO MAISHA
FURAHA LIJIKOSESHA
ILI KUNIFURAHISHA
WAKATI UKINILEA

MFANO TONE JANGWANI
ILIVYO YAKO THAMANI
CHA KUKULIPA SIONI
NI DUA KUKUOMBEA

NIKIKUPA DARAHIMA
AU MCHELE NA NYAMA
KATU DARAJA YA MAMA
HAZIWEZI KUFIKIA

NAKUTAKIA BAHATI
UPATE KAULI THABITI
NA KULE KWENYE SIRATI
UPITE BILA UDHIA

NAKUOMBEA KARIMA
UFUFULIWE NA WEMA
MARYAMU NA FATHWIMA
NA WOTE WALOBAKIA

MTUME MESISITIZA
TENA AMETUHIMIZA
WAMAMA KUWASIKIZA
KAMA ILIVYO SHERIA

SWAHIBU NIKUUSIE
MAMA NENDA KAMWAMBIE
RADHIZE AKUPATIE
KAMA ULIMKOSEA

MAMA ZETU TUWALEE
NA PEPO TUJIJENGEE
KWENYE NYUMBA ZA WAZEE
SIWAPELEKE SIKIA

UNAPOMKERA MAMA
UNAMUUDHI KARIMA
KESHO SIKU YA KIAMA
UTAENDA JIJUTIA

JIKAZE USIMUUDHI
ITAMBUE YAKE HADHI
ILI UIPATE RADHI
YA MAMA PIA JALIA

NAMUOMBA YA KARIMA
ANIPE NAMI UZIMA
NIMTUNZE WANGU MAMA
HADI MWISHO WA DUNIA

MWISHO WA LANGU SHAIRI
JINA LANGU NAKARIRI
NI FARWA WA HARIRI
KWAHERI NAWAAMBIA

1 thought on “MAMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *