HARUSI ZA MASHINDANO

      No Comments on HARUSI ZA MASHINDANO

Mwanangu ‘mepata heri, nikaha haiko mbali
Harusi ya kifahari, na tena ilio ghali
Nitamfanyia mwari, watu wakomeke kweli
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Kukopa nipo tayari, malaki mamilioni
Harusi iwe nzuri, sifa zijae pomoni
Kwa watu nijifakhiri, niwe mimi namba wani
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Harusi wiki nzima, liwe gumzo mtaani
Watu wapate kusema, na kusifu hadharani
Pesa nilizozithuma, nimalize harusini
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Nilikodishe holi, lilojengwa kwa vigae
holi milioni mbili, watu wote washangae
Wa karibu na wa mbali, waje wajimwae mwae
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Nilinunue veli, veli toka uturuki
Na tena liwe la ghali, veli halimithiliki
Nisifiwe kweli kweli, nao wote halaiki
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Na vyakula ainia, kuku, samaki na nyama
Viwe zaidi ya mia, tena vya kubwa gharama
Watu wakinisifia, nitapata kuterema
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Yeye kadi alitoa, kadi moja shingi mbili
Mimi nitamkomoa, nizichapishe za ghali
Watu watanitambua, nitheze harusi kweli
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Holi dera alitoa, mukaona ni ajabu
Basi mimi nawambia, nitaganyiza dhahabu
Kila anayeingia, atapewa bila tabu
Nataka fanya harusi, iishinde ya fulani

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *