Maneno ya tangu jadi, waliyanena waneni
Kwetu sisi ni zawadi, tuyatie akilini
Japo nyumba ya kukodi, ipambe nje na ndani
Hakika umaridadi, huficha umasikini
Tena ifukize udi, ingawa wa ishirini
Ipambe kwa mawaridi, japo ni ya hamsini
Na ‘curtaini’ ikizidi, ingawa za mtumbani
Hakika umaridadi, huficha umasikini
Tena lifahamu hili, lifahamu kwa makini
Si lazima nyingi mali, kujaza raha moyoni
Muhimu kujikubali, kujua yako thamani
Kuipamba yako hali, huficha umasikini
Isiwe utaparara, eti kisa masikini
Japo linunue dera, mia mbili hamsini
Kupendeza na kung’ara, si lazima milioni
Kukataa kucharara, huficha umasikini