Hujipinda muungwana, uvivu hueka kando
Vilivyo akapambana, akatenda kwa upendo
Wala haongei sana, na kuvifanya vishindo
Ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo
ashikiwakiswahili ❤️
Ni maneno ya hekima, maneno ya dhahabia
Wahenga waliyasema, mafunzo kutupatia
Tukiitaka salama, muhimu kuzingatia
Kila mcheka kilema, naye humsikilia
~ashikiwakiswahili
Kwa makini nimekaa, shairi niliandike
Shairi la manufaa, soteni tunufaike
Ya wahenga nimetwaa, nanyi ndugu muyashike
Hakika ya bovu paa, mtu hulizimba lake
~ashikiwakiswahili
Hawezi pata makini, wala hawezi tulia
Na mara yupo mbioni, jiko anakimbilia
Hamu yake akilini, chungu kukiangalia
Alo na chungu jikoni, haachi kuria ria
~ashikiwakiswahili