
Nawauliza wenzangu, la kimjadala swali
Hakika ya swali langu, laniumiza akili
Nijibuni wangu wangu, tupate jibu kamili
Ni yapi maji sahihi, ya kukandia chapati ?
Eti ni maji makali, yalopuliwa jikoni
Ndiyo siri ya ukweli, chapati kuwa laini
Wengine hawakubali, eti haiwezekani
Basi ni yapi sahihi, ya kukandia chapati?
Wengine eti hunena, maji ni ya uharara
Ni maji mazuri sana, chapatize ndio bora
Ukweli twakorogana, leo tupigeni kura
Tujue yalo sahihi, ya kukandia chapati
Na maji baridi pia, wapo walotia neno
Unga ukiyakandia, hupati shida mkono
Chapati zitabakia, laini kwa siku tano
Ni yapi maji sahihi, ya kukandia chapati?
~ashikiwakiswahili