
Ni kitamu Kiswahili, ndugu fahamuni
Utamu kama asali, umejaa ndani
Wengi wanakikubali, anopinga nani?
Kiswahili kitukuzwe!
Tukipende Kiswahili, na tukithamini
Tuwapo kila mahali, tukizungumzeni
Dharau tuweke mbali, kwenye lugha hini
Kiswahili kitukuzwe!
Ni ya kale lugha hii, zama za wahenga
Waliifanya bidii, lugha kuijenga
Basi na sisi tutii, kutoiboronga
Kiswahili kitukuzwe!
Kiswahili kinang’aa, na kinapendeza
Aidha kimesambaa, hadi uingereza
Kinakua kila saa, nimepeleleza
Kiswahili kitukuzwe!
~shairi lililochanganya bahari ya msuko na kikai
~ Malenga Farwa
Wenye kunena kunena mwacha mila ni mtumwa. Naam, lugha ya kiswahili ni lugha yetu. Ni lugha inayowakilisha utamaduni wetu na kubwa zaidi ni lugha inayoimarisha umoja wetu. Hivyo basi, ni muhimu kuikumbatia lugha hii na kukataa kata kata kuwa watumwa kwa kuitelekeza.
Vile vile lugha ya kiswahili ni lugha inayokua kwa kasi kubwa mno. Nchi nyingi zinafunza lugha hii kwenye shule sasa hivi. Si Afrika kusini, si Ulaya na kwengine kwingi. Wasiokuwa wenyeji wa lugha hii wameamua kuikumbatia na kuifanyia bidii lugha hii kwasababu wamegundua ladha na umuhimu wake. Sasa ni kwa nini sisi wenyeji tuitupe na tuionee aibu? Ni kwa nini tusiitukuze na kujivunia nayo? Wengi wetu tukisimama mbele ya hadhara tunataka tuongee kiingereza ili tuonekane wasomi. Hivi ni nani aliyesema lugha ya kiswahili ni lugha ya wasiosoma? Ni lini tutayabadilisha mawazo yetu kuhusu lugha hii adhwimu? Je tupo tayari kuja kupokonywa lugha hii kutoka kwenye viganja vyetu? Tuamke! Kwani tusipoitunza na kuimiliki lugha hii basi wapo watakaokuja kutufanyia kazi iliyotushinda.
Naam, kiswahili ni lugha tunayopaswa kuijenga na kuiendeleza kama walivyofanya mababu zetu. Nilipokuwa chuoni mwaka wangu wa mwisho yaani mwaka 2019, nilijiwa na wazo la kuanzisha shirika ambalo litaweza kuikuza lugha ya kiswahili. Kutokana na kwamba mimi ni ashiki shadidi wa lugha hii pendwa basi wazo hilo lilifurahisha hadi ya kunifurahisha na papo hapo nikawajuza watu wangu wa karibu na kuwataka ushauri. Nilipata majibu ya kutia moyo sana lakini kutokana na sababu za hapa na pale mwaka huu 2022 ndio nimeweza kulizindua shirika hili.
Sayari Ya Kiswahili (SAYAKI), ni shirika linalodhamiria kuikuza lugha ya kiswahili kutumia mbinu tofauti tofauti.
Naam, kiswahili ni lugha yetu na ni wajibu wetu kuitunza na kuikuza ili iweze kubaki, kukua na kuenea. Kupitia shirika hili nina imani kuwa lugha ya kiswahili na utamaduni wake utaweza kukua na kuwafikia wengi. Aidha tutaweza kubadalisha mawazo hasi kuhusu lugha ya kiswahili.