MWANANGU SIKUJUA

      No Comments on MWANANGU SIKUJUA

MWANANGU SIKUJUA
Machozi yaliokuwa yakitiririka kutoka kwenye macho ya mwanangu Sikujua yaliuvunja moyo wangu vipande vipande. Niliutazama uso wake uliodhihirisha upole, unyenyekevu na kutokuwa na hatia na moyo wangu ulizidi kuniuma. ‘Hivi hawa watu wanapata faida gani kumbwagia mwanangu lawama nzito kama hizi? Hivi wanaujua uchungu wa mwana? Tena mwana mpole, mwenye nidhamu na ambaye uso wake unadhirisha wazi kuwa hana hatia? Kwa nini wanashindwa kuuona ukweli kwenye macho yake?’
“Kwa hiyo mama nadhani umenifahamu vyema.”
Ghafla nilizunduliwa kutoka kwenye bahari ya mawazo na sauti ya mwalimu mkuu.
“ Sikujua tunampa adhabu ya kukaa nyumbani kwa miezi mitatu. Kesi ya kupatikana na bangi ni kesi yenye uzito mkubwa mno. Ilitakiwa afukuzwe kabisa shule lakini kwa sababu wanafunzi tumekwishawaandikisha kukalia mtihani mkuu tutamruhusu arudi kufanya mitihani yake.”
Niliuinua uso wangu uliokuwa umegeuka mwekundu kwa ghadhabu nikamtazama mwalimu mkuu hali nimemkazia macho. Nilitamani nimpige kibao kwenye uso wake uliojaa ndevu kama mtu mwenye hekima na busara lakini nikajikaza. Ndiyo wao wana roho za kinyama kiasi cha kumsingizia mwanafunzi jambo zito kama hilo lakini mimi sitojishusha kama wao. Abadaan sitoishusha hadhi yangu kujaribu kushindana na binadamu wasiojua utu. Niliinuka ghafla, nikamshika mwanangu mkono na kutoka kwenye ofisi hiyo.
“Lakini mama wananisingizia! Kuna mtu aliziweka hizo bangi kenye mkoba wangu. Mimi sina hatia. Nikikaa nyumbani kwa muda mrefu nitaanguka mtihani mama.” Sikujua alisema kwa sauti ya kuhurumisha.
Maneno yake yaliniumiza sana na huruma kunivaa lakini sikuwa na budi ila kuondoka na mwanangu katika sehemu hiyo ambayo utu hauthaminiki. Sehemu ambayo kwamba tuhuma hupachikwa yeyote tu bila uchunguzi wa kisawasawa kufanywa. Sehemu ambayo dhuluma ni jambo la kawaida tu na huruma ni kitu kilichogura kwenye nyoyo zao.
“Sikujua mwanangu umeshajieleza vya kutosha ila hakuna atakayekukuelewa hapa. Hakuna atakayekusikiliza na kukuonea japo chembe cha huruma. Tuondoke! Na hautarudi tena katika shule hii abadaan kataan.” Nilisema hali ya kuwa mori umenipanda maradufu na kutoka katika ofisi hiyo.
Sikujua alikuwa mwanangu wa kipekee niliyempenda na kumuenzi kama mboni ya jicho langu. Nilijitahidi sana kumpa mapenzi ya kutosha ili kuziba pengo la baba yake ambaye alitoweka nilipokuwa na ujauzito wake. Nilijifunga kibwebwe kumlinda kutokana na chuki na balaa za kilimwengu. Naam, alikuwa mwana mpole, msikivu na mwenye heshima kwangu. Wanafamilia na majirani walisema maneno mengi mabaya kumuhusu lakini niliwapuuzilia mbali. Nilifahamu kuwa ni wivu tu unaowasumbua kumuona mwanangu akiishi Maisha mazuri na kupata kila kitu alichokihitaji katika maisha yake licha ya kutokuwa na baba.
Ilikuwa asubuhi ya kupendeza. Niliamka mwingi wa furaha na uchangamfu. Nilisimama kwenye roshani ya chumba changu na kuwatizama wafanyikazi wachapakazi walivyokuwa wakiendelea na kazi zao katika ua wa nyumba yangu. Mwenye kusafisha bwawa la kuogelea alionyesha umbuji wake katika kufanya hivyo. Mwenye kukata nyasi naye alifanya hivyo kwa uzoefu mkubwa. Muosha gari vile vile aliosha kwa makini ili kuhakikisha hakubaki uchafu hata kiduchu. Kiukweli nilipendezwa mno na mandhari ya ua wangu. Maua ylichanua vizuri na kuongeza uzuri wa mandhari hayo. Nao videge vya kila rangi viliruka kutoka mti hadi mti. Nilikuwa nimezama kwenye uzuri wa ua wangu nilipozinduliwa ghafla na sauti ya Sikujua.
“Mama habari ya asubuhi.”
“Nzuri mwanangu kipenzi. Za wapi? Nakuona umependeza. Napenda sana unavyojisitiri unapotoka. Buibui limeziba umbo lako zuri maana mwanangu nawe umeumbwa ukaumbika, usije ukapeleka wanaume mbio huko nje.” Nilimwambia Sikujua tukacheka kwa pamoja kisha nikaendelea. “Kiukweli umevaa vizuri. Buibui lako pana na mtandio wako mkubwa. Najivunia sana kwako na ndiyo maana majirani wanakuonea gere kutokana na tabia yako adhwimu.”
“Ndiyo mama. Usiwasikilize wale watakutia presha bure. Mimi naenda kwa kina Sakina.”
“Sawa mwanangu. Kuwa makini.”
Muda mchache tu baada ya Sikujua kutoka. Jirani yangu Mariamu aliingia. Baada ya kujuliana hali alianza gumzo lake au tuuite wimbo wa taifa. Sikujua hivi, Sikujua vile.
“Mama Sikujua hivi umemuona mwanao alipotoka humu ndani? Umemruhusu kutoka vile?” Alisema Mariamu huku uso wake ukidhihirisha mshangao wa hali ya juu.
“Mbona sikuelewi.” Nilisema hali ya kuwa nimeshasinywa kwa sababu nilijua mazungumzo yalikokuwa yakielekea. Haya Sikujua amefanya nini tena? Ameua? Au ameteka nyara?”
“Nimepishana na Sikuju njiani nlipokuwa naja hapa. Hayo mavazi jamani.”
“Kuvaa buibui siku hizi ni hatia? Makubwa!”
“Buibui! SIkujua nimemuona akiwa amevaa nguo imembana na mtandio kauweka shingoni.”
“Sikujua ameniaga akiwa amevaa buibui na mtandio wake mkubwa. Kama huna la kusema ni vyema ukitoka nyumbani kwangu.”
“Tuachane na hayo, kuna siku ulipokuwa umesafiri na kumuacha mwanao peke yake, alianza kuingiza wanaume humu ndani.”
“Unauona ule mlango? Ulivyoingia kupitia mlango ule basi vivyo hivyo tafadhali toka. Kama huna maneno mengine isipokuwa kumzungumzia mwanangu tu basi usirudi tena katika nyumba hii. Nyumba hii uione paa!” Nilimfukuza jirani yule kwa hasira za mkizi.
“Lakini ujue mimi nakutakia mazuri na nampenda sana Sikujua ndiyo maana najaribu kukufungua macho ili usije kujuta baadae.” Alisema Maryamu huku akiitengeza kanga yake aliyofunga vyema kichwani.
“Nimesoma toka na tena usinifundishe kulea.” Mori ulinizidia nikamsukuma Mariamu nje na kuubamiza mlango.
Hakika nilichoshwa hadi ya kuchoshwa na maneno ya watu ya mara kwa mara. Hata dada yangu naye pia kila anaponitembelea mad ani Sikujua. Tukikutana kwenye duka kuu salamu ni Sikujua. Tukikutana harusini nyimbo ni sikujua. Alhasili ilikuwa ni maneno tumbi nzima kumuhusu mwanangu Sikujua. Watu walikuwa kana kwamba hawana shughuli za kufanya. Walitoka watokako guu mosi guu pili kuja kwangu kumsema Sikujua. Maneno yao niliyaona kero katika Maisha yangu na hivyobasi nililazimika kuchukua maamuzi mazito. Ndiyo! Niliamua kujiweka mbali na majirani pamoja na familia. Nilikata kabisa mawasiliano nao kwani niliona hiyo ndiyo njia salama ya kuepukana na maneno yao ya mara kwa mara.

“Hapana musimfanyie hivyo mwanangu.” Nilijaribu kuwarai wanaume wale makaktima waliokuwa wakitaka kumnajisi mwanangu. Hata hivyo, kilio changu kiliangukia kwenye sikio la kufa na bidii zangu kuambulia patupu. wanaume wale walimfanyia unyama mwanangu. Sikujua alilia kwa uchungu lakini hawakumuonea huruma. Baada ya kutenda ukatili huo walimuacha Sikujua akilia kwa uchungu na kutoroka.
Niligutuka kutoka usingizini na kufahamu kuwa ilikuwa tu ndoto. Moyo ulinienda mbio, kijasho chembamba kunitirika na mwili kunitetemka. Nilifurahi na kushusha pumzi kujua ya kwamba ilikuwa tu ndoto lakini pia nilikuwa na wasiwasi juu ya Sikujua. Niliinua simu na kupiga lakini haikupokelewa. Mapigo ya moyo nusura yasimame. Nilipiga tena lakini haikupokelewa. Nilisimama kutoka kitandani na kuanza kutembea chumba kizima kama mama mwenye uchungu wa kuzaa. Akili iliwaza hili ikiwacha lile. Ghafla mlango ulifunguliwa na Sikujua akaingia.
“Wewe mbona ulikuwa hupokei simu? Unataka kuniua?” Nilissema huku mori umenipanda.
“Mama kwani kuna nini? Mbona uko hivyo? Sikushika simu kwasababu nilikuwa chini kwenye geti kwa hiyo nikaona maadamu nishafika nyumbani hakuna haja kushika nikakumalizia salio la simu.”
“Upo salama lakini?” Nilimkumbatia mwanangu na kupata amani na faraja.

Ilikuwa ni harusi ya swahiba yake Sikujua. Sikujua alijitayarisha na kwenda katika harusi hiyo. Cha kushangaza ni kuwa Sikujua alirudi nyumbani mapema sana bila shaka kabla ya harusi kwisha. Alikuwa akilia huku nguo yake imechanika na kujaa vumbi. Aliingia moja kwa moja kwenye chumba chake na kujifungia. Nilijaribu kadri ya uwezo wangu kumbembeleza ili atoke na kunieleza yaliyomsibu lakini wapi! Niliingiwa na wasiwasi kupita maelezo. Tukio hilo lilinitia kimbimbi na niliogopa hata kufikiria. Niliogopa kuwaza yaliyomsibu Sikujua. Hata hivyo akili yangu ilinisaliti na kuwaza vitu vya ajabu. Subira iliniishia na kuamua kuwaita wafanyikazi wangu kunisaidia kuuvunja mlango wa chumba hicho. Nilimkuta Sikujua amejibanza kipembeni akilia. Nilihofia kumuuliza yaliyomsibu. Nilihisi moyo wangu haupo tayari kupokea habari mbaya kwani kwa hali ilivyoonekana tukio lililotokea ni kubwa. Nilihofia kuwa nisingeweza kuhimili uzito wa Habari zenyewe lakini sikuwa na budi. Lisilobudi hubidi ebo! Nilimuuliza Sikujua kwa sauti yenye wingi wa wasiwasi.
“Umepatikana na nini mwanangu?”
“Nimenajisiwa mama!” Alijibu Sikujua akanikumbatia.
Nilizimia!
Niliregelewa na fahamu baada ya saa kadhaa na jambo lililonijia akilini ni kumpeleka Sikujua hospitali kufanyiwa vipimo na kutibiwa. Hata hivyo, Sikujua alikataa kata kata kutokana na aibu iliyomvaa. Niliona hatua ya pili ni kwenda mahakamani lakini kwanza nilipaswa kumfahamu mwanamume kakatima aliyemtendea mwanangu unyama huo. Kwa bahati nzuri Sikujua alimfahamu vyema mwanamume huyo na pia alapajua anapoishi. Nilimtafuta wakili bora nchini na kumlipa kiwango kikubwa cha pesa ili tu mwanangu apate haki. Wakili huyo alisema Ushahidi mkubwa ni Sikujua kufanyiwa vipimo hospitalini tena haraka iwezekanavyo. Hata hivyo, Sikujua alikataa kata kata kwenda hospitalini. Alijifungia chumbani na kukataa kutoka. Nilijaribu kadri ya uwezo wangu kumshawishi na hatimaye akakubali.
“Vipimo vinaonyesha kuwa Sikujua hajanajisiwa.” Daktari alisema.
“Inawezekana vipi daktarin? Mwanangu ameharibiwa Maisha alafu unaongea nini sasa!” Nilisema kwa ghadhabu.
“Nimefanya vipimo kwa makini san ana hayo ndiyo matokeo.” Alissisitiza daktari.
“Mama inawezekana vipi lakini? Mimi ni…..me…ni…me….najisiwa mama.” Alisema Sikujua akilia kwa uchungu.
“Nakuelewa mwanangu. Usijali lazima utapata haki. Daktari basi tusipoteze muda nakuomba utengeze matokeo bandia. Nitakulipa kiasi chochote cha pesa unachotaka.”
“Hapana! Hicho ni kinyume na kazi yangu. Siwezi kufanya hivyo.” Alisema daktari.
“Sasa unasemaje.” Nilimwangalia daktari huku nikiweka bunda la pesa kwenye meza.
Daktari bila kusita alitengeza matokeo bandia.

Kesi ilianza mahakamani. Nilikaa pamoja na mwanangu huku nimemkumbatia kwasababu alikuwa anapitia wakati mgumu. Mshtakiwa aliitwa kizimbani na akasimama huku akitizama chini. Alikuwa na sura ya upole sana na macho yake yalikaa kuhurumisha. ‘kumbe mtu katili anaweza kujihurumisha kiasi hichi. Huyu mwanamume ukimuona utadhani ni mstaarabu na mwenye maadili kumbe ni katili.’ Mawazo yalisongamana akilini mwangu huku nikimuangalia mwanamume yule kwa hasira. Alijitahidi sana kujitetea na wakili wake pia alifanya kila hali lakini wakili wangu aliwashinda akili. Aliendesha kesi vizuri na kutoa ushuhuda kamili ambao usingeweza kupingika. Naam, alikuwa wakili mwenye uzoefu na ushuhuda wa daktarin ulikuwa ushuhuda mzito.
“Mshtakiwa umepatikana na hatia yakumnajisi Sikujua Mashauri siku ya jumamosi tarehe ishirini mbili, Oktoba mwaka elfu mbili na ishirini. Umepewa hukumu ya miaka mitano jela na fidia ya shilingi laki tano kwa muathiriwa kwa kumuharibia maisha yake.” Alisema jaji mkuu .
Nilipata faraja baada ya kuona kuwa mwanangu amepata haki. Tulirudi nyumbani tukiwa na amani japo niliumia sana kujua kuwa mwanangu ataishi na kumbukumbu za tukio hilokatika Maisha yake yote. Niliiona huzuni usoni mwake hata baada ya kutoka mahakamani. Nilijaribu kumliwaza lakini alitabasamu tu na niliona wazi kuwa tabasamu lile lilikua bandia.
Miezi ilipita baada ya tukio hilo na nilikuwa nimeketi sebuleni nikitizama Habari. Habari ya kwanza kabisa ilikuwa ya mwanamke aliyenajisiwa na wanaume watatu. Habari ile iliniuma sana hasa nilipofikiria kuwa kitendo kile kiliwahi kumfika mwanangu. Ghafla simuya Sikujua iliita na yeye alikuwa msalani. Iliita mara ya pili, mara ya tatu na hatimaye nikaamu kuipokea. Nilipoipokea tu hivi ilikatika nah apo hapo kukaingia ujumbe mfupi. Sikuwa na mazoea ya kusoma jumbe za mwanangu lakini nilijikuta naufungua ujumbe huo.
“Swahiba tumemfundisha adabu yule anayejifanya janadume. Eti kakubaka, unaanzaje kubakwa kwa mfano hahaha…basi shika simu swahiba nikupashe.”
Ujumbe huo ulinshtua kupita maelezo. Moyo ulinidunda na jasho kunitiririka.Niliingiwa nah amu ya kusoma jumbe zaidi. Nilisoma jumbe za awali.
“Hamisi si amekataa kukuoa baada ya kuuvunja moyo wako? Waonaje tumfundishe adabu kwa kumsingizia kesi ya kubaka. Muache akaozee jela ajue sisi si watu wa kuchezewa.”
“Mama ana pesa kama njugu, kesi nayo lazima tushinde na mimi wanijua tena, gwiji katika kuigiza.”
“Hivi ulikuwaje mzembe mpaka bangi zikapatikana kwenye begi langu? Si nilikwambia uzifiche chini ya kitanda?”
“Buibui la nini nawe! Wewe livae ukitoka nyumbani ukifika njiani livulie mbali. Uvae buibui alafu uzuri wako watauonaje?”
Nilishindwa kuendelea kuzisoma jumbe hizo. Simu iliniponyoka. Machozi yalinitiririka njia mbili mbili. Moyo ulivunjika vipande vidogo vidogo. Nilishindwa kabisa kuyaamini niliyoyasoma. Sikujua mwanangu! Mwana nilyiyempenda na kumuamini. Mwana niliyemtetea kwa kila hali. Nimeteta na ndugu na majirani kwa sababu sikujua ukweli. Sikujua yaliyokuwa yakiendelea. Sikujua kuwa ninamlea mwana asiyekuwa na maadili hata kdogo. Nilishindwa kuuona ukweli uliokuwa mbele ya macho yangu. Mapenzi ya mwanangu yalinipofusha. Nitawakabili vipi watu? Nitawakabili vipi ndugu na majirani waliokuwa wakinitakia heri? Niliwaona maadui kumbe walikuwa marafiki wa dhati waliojaribu kunitoa kwenye shimo lenye kiza totoro. Ndiyo! Si vizuri kuyafuata maneno ya watu lakini kuyasikilizani muhimu. Ni muhimu kuyasikiliza yale unayoambiwa, ukayafanyia uchunguzi na kuaminina kuyatendea kazi yale yenye ukweli ndani yake. Yaani mimi nimemfunga jela kijana wa watu asiyekuwana hatia? Hakika nimefeli! Nimefeli kama mama! Nimefeli kwa mwanangu!
Sikujua alirudi kutoka msalani na kunikuta nikilia huku simu yake imeangukia miguuni. Aliichukua simu na kuziona zile jumbe.Aliniangukia miguuni na kuomba radhi,
“Mama nisamehe!”
“Sikujua umeniangusha! Sio wewewa kuniomba mimi msamaha. Mimi ndiye ninayepaswa kukuomba wewe msamaha kwa kushindwa kukupa malezi mema. Nilikupenda kupitiliza na ukaamua kuyachezea mapenzi yangu mchezo. Umenisaliti Sikujua. Umeniumiza. Umeniangusha. Unazungumzia msamaha? Vipi kuhusu kijana ambaye kwa sasa hivi yupo jela anateseka bila hatia? Msamha utaniomba mimi au yeye? Hakika mwanangu Sikujua ninaishi na mbwa mwitu aliyejivisha ngozi ya kondoo. Sikujua!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *