
Ya ilahi ya wadudi, Mola wetu subuhana
Tujaalie suudi, na siku yetu kufana
Litimu letu kusudi, na kufurahia sana
Kuleta hini zawadi, kwa huyu wetu kijana
Leo nipo furahani, wewe kukuzawadia
Na pete hini chandani, Sharifa nakupatia
Watu tushangilieni, vigelegele kutoa
Kwa furaha tuthezeni, Siku njema kutujia
Siku tuliongoja, imefika kwa salama
Nakutakia faraja, na furaha ya daima
Ilete njema natija, ndoa yako iwe njema
Uishi kama Khadija, naye mumewe Hashima
Umefanya njema kazi, sote ‘metufurahisha
Sharifa wetu kipenzi, hadhi umetupandisha
Mama Halima mzazi, Leo ‘memuheshimisha
Basi leo wazi wazi, pete ninakuvalisha
Maisha yalo murua, sharifa nakutakia
Matamu kama halua, na tena ya kuvutia
Ndoani ukiingia, neema kukushukia
Niliyekuzawadia, ni mimi bibi Asia