Mno nilifurahia, kuliona paa langu
Sana nilijivunia, haivuji nyumba yangu
Paa lilotulia, kalijenga fundi wangu
Sikujua kukinyesha, nitaona pavujapao
Jua lilijiwakia, paa tatizo halina
Mno lilinivutia, nikafurahia sana
Kila ‘kiliangalia, kasoro sikuiona
Sikujua kukinyesha, nitaona pavujapo
Siku moja ikafika, mvua ikajinyia
Maji yalitiririka, nyumbani yakaingia
Mno nilihuzunika, vyombo ‘liniharibia
Sikujua kukinyesha, nitajua pavujapo
Kumbe lina tundu paa, sana linajivujia
Hakika nilishangaa, hilo sikutarajia
Paa ‘meleta balaa, funzo limenipatia
Sikujua kukinyesha, nitaona pavujapo
Ingawa nimeumia, na kunitanda huzuni
Mno ‘mejishukuria, kujionea machoni
Paa lilonivutia, nimelijua undani
Afadhali kumenyesha, nikajua pavujapo
~ashikiwakiswahili
Shairi zuri MashaAllah
Shukran malenga 🙌