UTENZI WA RAMADHAN

      No Comments on UTENZI WA RAMADHAN

Leo hii ni ya kwanda
Tuwe wenye kujipinda
Tufanye ano yapenda
Na kumridhi jalia

Tumuombeni jalali
Mchana pia laili
Na kila tunaposwali
Atujaalie afia

Tufunge bila usiri
Tena kwa nyingi sururi
Tupate yalo mazuri
Mola ‘lotuandalia

Tutieni moja nia
Kuwa tutajifungia
Kwa ikhlasi na nia
Na unyenyekevu pia

Nayo pia qurani
Kwa hima tuisomeni
Juzu tukamilisheni
Japo mara wahidia

Ni Ramadhani ya pili
Tumuombeni jalali
Atupe nasi sahali
Tufunge bila udhia

Maaswia tuacheni
Kheri nyingi tufanyeni
Usiku tuamkeni
Ibada kujifanyia

Tusipotezeni muda
Kufanya yaso faida
Bali tufanye ibada
Hiyo ndio sawa ndia

Ni mwezi wa kuyachuma
Mambo mengi yalo mema
Basi tufanyeni hima
Thawabu kujipatia

Pia tushikeni hamu
Kuacha yalo haramu
Kwani hini ni awamu
Ya kutengea tabia

Imewadia ya tatu
Kuasi tusisubutu
Tusafishe nyoyo zetu
Tufuate sawa njia

Tuchukueni sabuni
Nyoyo zetu tuosheni
Nyeupe tuzifanyeni
Zitatengea tabia

Tuwe sana wakarimu
Daima tutabasamu
Tupendaneni kaumu
Na kuswafiana nia

Pia sana tutoeni
Tukumbuke masikini
Toa japo ishirini
Au hata moja mia

Imewadia ya nne
Mema tuamrishane
Zaidi tuhimizane
Maovu kuyakimbia

Na mikono tushikane
Pema tuelekezane
Wengine tusitukane
Na tukajiharibia

Msaada tupeane
Mazuri tuambiane
Katu tusipotoshane
Tukaja potea njia

Enyi ndugu tupendane
Tuloteta tupatane
Usiku tuamshane
Ibada kujifanyia

Pia sana tung’ang’ane
Ibadani tushindane
Thawabu zipatikane
Ziwe mia kwa mamia

Leo tano Ramadhani
Kamba tukaze jamani
Tuzameni ibadani
Thawabu kujichumia

Tuleteni adhkari
Usiku pia nahari
Tuseme yalo mazuri
Maovu kuyakimbia

Darasa tusikilize
Mambo mema tujifunze
Katu damu tusilaze
Mazuri kujifanyia

Sadaka tutoe sana
Vyema kusaidiana
‘tatubariki rabana
‘Kifuata sawa njia

Ya sita imewasili
Shukurani kwa jalali
Kuzidi tupa sahali
Saumu kujifungia

Tuzidi sana kuswali
Kwa ikhlasi ya kweli
Maovu tuweke mbali
Tuzidi kuyakimbia

Pia swala za laili
Tuamkeni tuswali
Ndio mwendo wa rasuli
Nao maswahaba pia

Tufanye yalo mazuri
Tena kwa hamu na ari
Maovu tutahadhari
Yasije tuharibia

Ya sabaa imefika
Kwa uwezo wa Rabuka
Kamba tuzidi kushika
Tusije iachilia

Tusipoteze wakati
Jikoni sana kuketi
Kuzipika kaimati
Na vyakula ainia

Na sana tujitahidi
Tuweze kuzifaidi
Za Ramadhani zawadi
Mola ‘lotuandalia

Tusikubali kabisa
Fadhla nyingi kuzikosa
Hivyo tuache mikasa
Itayotuharibia

Ni ya nane Ramadhani
Shukurani kwa manani
Kututia uzimani
Tuna siha na afia

Fursa tuitumieni
Kuzizidisha imani
Na tujirekebisheni
Ziwe nzuri tabia

Miraa tuiacheni
Sigara tusivuteni
Nayo pombe tusinyweni
Mchana usiku pia

Tabia tuache nyuma
Zile zisizo njema
Tufuate mwendo mwema
Mwendo wa wetu nabia

Kwa uwezo wa Rahimu
Ya tisia imetimu
Tuifungeni saumu
Kwa ilio safi nia

Tupunguzeni kulala
Tuamkeni laila
Na kusimamisha swala
Tutubuni sana pia

Tuamkeni suhuri
Karibu na alfajiri
Ndio suna ya bashiri
Tusiwe tutapuzia

Ya kumi ni leo hii
Basi tufanye bidii
Mola tuzidi mtii
Tusichoke nawambia

Hakika ya mwezi huu
Fadhila zipo ni kuu
Tusije tukala huu
Mema kutojifanyia

Tufanye kwa kila hali
Aturidhie jalali
Na adhabu kali kali
Mola ‘tatuepushia

Tuzishindeni nafusi
Tuyaepuke maasi
Tumuombeni Qudusi
Atuonye sawa ndia

Kwa furaha tulianza
Sasa kumi ‘memaliza
Basi tusije legeza
Kamba tukaachilia

Leo ni kumi na moja
Tujizatitini waja
Ili tuone natija
Mwishoni tukifikia

Kwa wingi tukisomeni
Kitabu chenye thamani
Si kingine Qurani
Nazidi kuhimizia

Adhkari tusomeni
Asubuhi na jioni
Nyoyo ‘tapata amani
Na pia kufurahia

Shukurani kwa jalali
‘Mefika kumi na mbili
Tuache lile na hili
Tufunge kwa safi nia

Kwa safi nia tufunge
Pia vyema tujipange
Mengi mema tuyachange
Mizani kujijazia

Ziwe nzito mizani
Tufikapo hisabuni
Mwisho tungie peponi
Tukawe naye nabia

Basi tufanyeni hima
Tujitahidi kuchuma
Mengi mengi yalo mema
Sadaka na zaka pia

Atujaalie Wahabu
Qiyama ‘sipate tabu
Tuvipokee vitabu
Kwa mkono wa kulia

Leo ni kumi na tatu
Tusafishe nyoyo zetu
Tuitoe yote kutu
Turekebishe tabia

Mwenendo uwe mzuri
Tuzifanye nyingi kheri
Adhabu zote na nari
Mola ‘tatuepushia

Tuzidisheni juhudi
Tumuombeni Wadudi
Sisi sote atuhidi
Kwenye ilo sawa njia

Kumi na nne yaumu
Ndugu tushikane hamu
Kuyaacha ya haramu
Halali kukumbatia

Tuifungeni saumu
Kwenye ibada tudumu
Tutapata ladha tamu
Ya imani nawambia

Tuweni na ikhlasi
Riya tuseme ni basi
Na malipo kwa Qudusi
Tuwe tutatarajia

Leo ni kumi na tano
Tuyaache magombano
Kutoleana maneno
Na kutukanana pia

Tusiweni tutateta
Na kuvieneza vita
Na kizazi kukita
Hizo si njema tabia

Tuishi kwa itifaki
Tuzitoe zote chuki
Upendo uwe wa haki
Nyoyo zutafurahia

Kumi na sita ‘mefika
Tuzitengeze huluka
Nazo Radhi za Rabuka
Tuwe tutajipatia

Mwenendo wake Hashima
Kiigizo chetu chema
Tufuate hima hima
Hiyo ndiyo sawa njia

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *