TUSAMEHEANE

      No Comments on TUSAMEHEANE

Ninaandika nudhumu, nyie kuwaleteeni
Naanza kutakalamu, masikio tegeeni
Ninaanza kwa salamu, nawaomba pokeeni
Msamaha ni muhimu, ndugu zangu fahamuni
Tusameheane!

Binafsi nawaombeni, munisamehe ndu yenu
Kama ‘meziumizeni, za ndani hisia zenu
Leo hii nipo chini, ninaomba radhi zenu
Basi nisameheeni, kwa dhati ya nyoyo zenu
Tusameheane!

Nyoyo tuzisafisheni, na kuzijaza upendo
Chuki tuziondoeni, kabisa tueke kando
Aidha tupendaneni, tuache vingi vishindo
Na tusameheaneni, ni wake mtume mwendo
Tusameheane!

Chuki hazina maana, tujaribu kuepuka
Tutaposameheana, nyoyo zitafurahika
Upendo ni raha sana, hilo na halina shaka
Wazee pia vijana, tuishi kwa itifaka
Tusameheane!

Husamehe rahmani, kwake tunaporejea
Tukiomba kwa imani, ghafuri hutupokea
Seuze sisi jamani, kitu gani twangojea
Na tusameheaneni, amani itaenea
Tusameheane!

Hapa mwisho nimefika, shukurani ni kwa Mungu
Natumai umefika, ‘lowapa ujumbe wangu
Kabla ya hapa kutoka, nawambia ndugu zangu
‘Mewasamehe hakika, kwa dhati ya moyo wangu
Tusameheane!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *