MKE MWEMA

      2 Comments on MKE MWEMA

Amesema mtume rehma na amani zimshukie, “dunia ni starehe na bora ya starehe zake ni mke mwema.”

Hapa mwanzo naanzia, kutunga yangu nudhuma
Natoa wangu wasia, uwafikieni umma
Hakika ametwambia, mtume wetu hashima
Starehe ya dunia, ni kupata mke mwema

Mke aliyetulia, ni raha ‘kimtazama
Hariri yake tabia, kwenye dini amezama
Mke aso na udhia, tena mwingi wa hekima
‘Tastarehe sikia, ukipata mke mwema

Mke anosubiria, huku akitabasama
Mazito munopitia, hukutuliza mtima
Si mwenye kukimbilia, “talaka yangu” kusema
Ndugu utafurahia, ukipata mke mwema

Unapopata simanzi, mawazo kikugandama
Mke wako laazizi, kando yako husimama
Akawa ni kitulizi, akawa nawe daima
Utapata raha hizi, ukioa mke mwema

Daima hukupeleka, kwenye njia ilo njema
Mkono akakushika, kuyatenda yalo mema
Na lau ukianguka, hukuinua kwa hima
Ukitaka furahika, basi oa mke mwema

Maneno yake laini, maneno yenye hekima
Yalotiwa asumini, na kupangiliwa vyema
Hatoi mwake kinywani, isipokuwa neno jema
Tajihisi u peponi, ‘kimpata mke mwema

Ni mwingi wa msamaha, umkerapo mtima
Ukamtia karaha, kumfanyia yaso mema
Ukiomba msamaha, hukusamehe daima
Ni raha jama si raha, kumpata mke mwema?

Na muda ukifikia, muda wake kuwa mama
Watoto wanakulia, kwa malezi yake mema
Dini na pia tabia, huwafunza hima hima
Moyo wako ‘tatulia, ‘kimpata mke mwema

Nimefikia mwishoni, naomba hapa kukoma
Dua nawaombeeni, muwapate wake wema
Wawe ni wenu wendani, mupendaneni daima
Wawe wenu hurulaini, kesho kwenye pepo njema

ashiki wa kiswahili
Farwat
4/4/2020

2 thoughts on “MKE MWEMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *