JANGA LA KORONA

      2 Comments on JANGA LA KORONA

Mie nimerudi tena, tungo kuwaleteeni
Ni tungo ilo bayana, kwa makini sikizeni
Ila naumia sana, na kunitanda huzuni
Hili janga la korona, ‘metutia maswalini
Ewe Mola Subuhana, twakuomba tuauni

Limepenya kila kona, kote kote duniani
Si ufaransa si China, limefika sikizani
Haibagui korona, watu wote mashakani
linatisha waungwana, ‘mejionea nadhani
Ewe Mola Subuhana, tuingize shifaani

Jamani hiki kirusi, ‘metuacha taabani
Kinasambaa kwa kasi, kama moto wa nyikani
‘Meenea wasiwasi, kote kote duniani
Wauliza adinasi, jama kitakwisha lini
Twakuomba ya Qudusi, tuingize salamani

Ni janga lenye kutisha, ‘mejionea wendani
Na pia lahuzunisha, ‘metutoa furahani
Kweli latuhangaisha, kote hadi Marekani
Lini hili litakwisha, jibu halionekani
Hakuna wa kutuvusha, isipokuwa Manani

Kiukweli inauma, hakwendewi msikitini
Kina baba kina mama, kuswaliwa ni nyumbani
Aidha  swala ya juma, haiswaliwi jamani
Ndugu turudini nyuma, maghfira tuombeni
Tumuombe ya Karima, atutoe mashakani

Ukifungua habari, habari ni za korona
Mazungumzo si siri, ni korona kila kona
Ugonjwa umeshamiri, nyie wote mumeona
Basi jambo lilo zuri, kumuomba Maulana
Iondoke yaa Qahari, korona ‘sirudi tena

Iwe ni funzo korona, kote kote duniani
Maaswia kila aina, jamani tuyaacheni
Ufisadi na hiyana, tuzifukie shimoni
Tuombeni toba sana, usiku tuamkeni
Na in shaa Allah Subuhana, atatupa afueni

Twakuomba yaa Rabuka, waja wako tupo chini
Janga hili kuondoka, lisirudi asilani
Tuwe ni wenye kuvuka, salama wa salmini
Tuweze tena kutoka, twende shule na kazini
Ya latifu yaa Rabuka, tuingize shifaani

Mwisho wa yangu nudhuma, nanga mie naitia
Natumai nyote umma, ujumbe ‘mewafikia
La muhimu ni uzima, Allah atupe afia
Na ienee salama, furaha amani pia
Farwa ni yangu isima, niite ‘taitikia

❤ashiki wa kiswahili ❤

🌹Farwat🌹

2 thoughts on “JANGA LA KORONA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *