MKE WA HERI

      2 Comments on MKE WA HERI

Heri alishindwa kabisa kuyatoa mawazo yake kwa binti yule. Binti mpole, mstaarabu na mkarimu. Binti ambaye kwamba pengine neno kununa halikupatikani katika kamusi yake ya maisha. Kila wakati alionekana akitabasamu na kudhihirisha vidu katika mashavu yake vilivoizidisha haiba yake ya kike. Haya yote yalicheza densi katika kichwa cha Heri na kumjaza mawazo ndi! Wakati mwengine alionekana akitabasamu peke yake na kutingisha kichwa. Mara alionekana kanywea na huzuni kumtawala .Mara alisikika akiimba mashairi ya kimahaba kwa sauti yake ya kumtoa nyoka pangoni. Alhasili alikuwa akielea katika dunia aliyoifahamu yeye mwenyewe.

Heri anaikumbuka vyema siku alipokuwa katika harakati zake za kutafuta riziki pale markiti. Shati lake jeusi alilovaa lililowa jasho chapa chapa kutokana na jua kali la Mombasa. Kichwani alivaa kofia nyeupe iliyoendana vyema na ndevu pamoja na sharafa zake zilizonyolewa kiufundi na kuambata katika ngozi nyeusi yenye mng’ao wa mbali.
“Saidi una manjano hapo?”
“Ndiyo yapo Heri.”
“Basi mpimie huyu mama tafadhali yangu yameisha. Mama nenda kwa yule pale utapata manjano. ”
Biashara ilikuwa imepamba moto alipokuja binti aliyeandamana na mama yake.
“Assalam alaikum!” Alisalimia binti yule huku akishika shika viungo vilivyokuwa kwenye ndoo na kuvinusa.
“Waalaikum salam!” Aliitikia Heri na mara adrenalini ilitolewa na mwili wake na moyo ukaanza kumuenda mbio.
“Pilipili manga nusu kilo bei gani?” Aliuliza binti yule kwa upole na ustaarabu huku wajihi umemkunjuka bila dalili ya kuwa ashawahi kununa katika maisha yake. “Kaka pilipili manga bei gani?” Ilibidi binti arejelee swali lake baada ya kumuona muuzaji ametoweka sehemu ile na kubaki mwili tu.
“Aah…..mmh…samahani…unasema? ”
“Pilipili manga nusu kilo ni bei gani?”
“Mia mbili hamsini. ”
Ghafla kulipita mtu aliyebeba gunia la viazi na kumpiga kikumbo binti yule.
“Rukia sogea sogea.” Mama yake binti yule alisema huku akimshika mwanawe.
Rukia alitabasamu tu na kusogea kando.
Heri alizidi kuchanganyikiwa kutokana na tabia ya binti yule ya kutokasirika. Alimfungia pilipili manga yake na kumkabidhi. Rukia alitoa mia tano naye Heri akamrejeshea baki yake kama mia saba hamsini.
“Nimekupa mia tano kaka.”
Loh! Heri aliona mambo yanazidi kwenda msegemnege. Alijaribu kushusha pumzi na kujituliza lakini wapi! Rukia na mama yake walipokea baki yao sahihi na kushika sabili kuelekea walikokuwa wakielekea. Mara palitokea msichana mdogo aliyewaomba kina rukia pesa.
“Mama tusimpe pesa heri tumnunulie chakula huyu.” Alisema Rukia huku akimpapasa yule mtoto kichwani. Heri alizidi kuvutiwa kutokana na ukarimu na hekima ya Rukia. Alipendezwa naye punde tu alipomuona na hulka zake zilizofuata zilimfanya avutiwe zaidi.

Adhuhuri ilifika na Heri alifunga funga biashara na kuelekea mskitini ili awahi jamaa. Siku hiyo alikaa muda mrefu zaidi kuliko kawaida yake. Aliomba dua kama kawaida yake lakini dua ya hiyo siku ilikuwa na utofauti. Ilikuwa dua ndefu zaidi na hakuomba yale aliyokuwa akiomba kila siku bali alijikita katika jambo moja tu. Alimuomba Mungu amsahilishie ampate yule binti ili amuoe. Aliomba kwa dhati apate mke wa heri. Baada ya hapo aliamua kurudi chengoni kwa sababu alihofia kutia hasara katika biashara yake kutokana na akili yake kutofanya kazi vizuri siku hiyo.

Kwa siku ayami Heri aliendelea kuwaza usiku kucha mchana kutwa ni jinsi gani angempata Rukia. Hakujua chochote kumuhusu. Alichokifahamu ni jina tu. Jambo hilo lilimuumiza sana kichwa na ghafla huzuni ikamtawala. Alilitazama paa la nyumba yake la makuti kana kwamba lilikuwa na majibu ya maswali yake. Macho yake yaliendelea kukitalii chumba na ghafla yakakutana na ufa kwenye ukuta, kisha alikitizama kitanda chake na godoro lilokuwa jembamba kama chapati. Alitabasamu na kuwaza, ‘Mbona nawaza vitu ambavyo kwamba nina hakika ni muhali kuvipata. Umaskini umeniandama na kunigandama. Kuna mke atakayenikubali mimi mlalahoi?’ Mara machozi yalimbubujika Heri na moyo wake kumuuma. ‘Lakini nina imani kama ni mke wa Heri, kwa uwezo wake Mungu bila shaka nitampata’. Aliweza kujifariji hatimaye.

Mawazo ya Rukia yalizidi kumsumbua Heri. Hivyo basi, aliamua kwenda kwa rafiki yake, Omari ili kumtaka ushauri.
“Aaah Rukia? Rukia Salim? Huyo mbona ni jirani yetu. Mfupi, mweupe na mama yake mnene mrefu?” Alisema Omari kwa yakini.
“Haswa!” Aliitikia Heri furaha imemjaa kama aliyeanguliwa mwezi. “Lakini Omari kuna uwezekano huenda siye.” Hapo tena huzuni na wasiwasi zilimvaa Heri.
“Tutathibitisha kwanza kabla hujamtuma mamako, sawa?”
“Sawa kaka.” Aliitikia Heri nusu mwenye matumaini nusu mwenye taharuki mbivu.

Omari alimpeleka Heri mpaka katika nyumba ambayo aliifahamu kuwa ni ya kina Rukia. Lilikuwa jumba kubwa na la kifahari lenye geti kubwa na ua wa kupendeza. Heri moyo ulimvunjika vipande vipande alipoiona hali ile. Alijiona kuwa hana hadhi hata ya kuwa mlinzi pale seuze mume.
“Ndiyo yule Rukia.” Omari aliuvunja ukimya uliokuwa umetawala kwa kipindi hicho kisha akamvuta Heri kwa kando ili wasionekane.
“Aaah ndiye yule niliyemuona Markiti huyu.” Alisema Heri tabasamu imemvaa.
“Baaaaaaaas! Tushathibitisha sasa. Hiyo ni hatua ya kwanza. Sasa fanya mpango umuelezee mamako suala hili kisha umtume huku.”
“Subiri kidogo Omari. ” Alisema Heri kama aliyekumbuka kitu. “Una hakika huyu binti hajaolewa?”
“Hapana hajaolewa kwa sababu hapa ni kwao anaishi na wazazi wake. Ingekuwa ameolewa bila shaka angeishi kwa mumewe.”
“Sawa basi Omari nitakuja na mama yangu kesho japo nina hofu sana. ”
“Usihofu kaka. Kinachohitajika hapa ni wewe ufanye juhudi zako kisha mengine muachie Mungu.” Omari alimfariji rafikiye, akampiga pambaja kisha kila mtu akashika njia yake.

Heri hakusita kumpa mama yake habari hiyo na kuhusu kwenda kwa kina Rukia.
“Unamfahamu vyema binti mwenyewe mwanangu? Kumbuka vyote ving’aavyo si dhahabu. ” Alisema mamake mtu mwingi wa busara.
“Rukia mama! Rukia! Rukia ni binti ambaye kwamba kwa dakika chache nimeweza kumsoma na kumuelewa kinaganaga mama.” Alisema Heri huku akimshika mamake mkono.
“Mmh! Heri mwanangu na je umeswali istihara?”
“Hilo kwa kweli nililisahau lakini nimemuomba sana Mungu kama ni mke wa heri basi nimpate bila pingamizi. ”
Sawa basi jitayarishe baada ya swala ya alasiri twende.
Heri alilitafuta shati lake aliloenzi na suruali yake alioletewa na rafiki yake kutoka Dubai. Alizipiga pasi kutumia pasi lake la makaa na kuzipaka mafuta mazuri ambayo pia yalitoka Dubai. Alizichana nywele zake barabara na kuivaa kofia yake ya vitho.

“Unaitwa nani? Je unafahamiana na Rukia?” Aliuliza mlinzi wa jumba la kina Rukia.
“Hapana.” Alijibu Heri hali amestaajabu kutokana na utaratibu wa jumba lile
“Madam kuna mgeni wako. Hapana hajawai fika hapa. Nimru…ooh nimruhusu? Amesema anitwa Heri….aaah hapana …..haya sawa madam. ” Alipiga simu mlinzi na hatimaye Heri na mamake waliruhusiwa kuingia baada ya kuacha vitambulisho vyao.
Walifika katika jumba hilo na kukaribishwa ndani na binti mdogo aliyevaa aproni. Baada ya muda mchache mama mwenye nyumba alifika sebuleni.
“Assalam alaikum! Karibuni mukae.” Alisema mama mwenye nyumba baada ya kuwaona wageni bado wamesimama tutwe.
“Asante.” Aliitika Heri na mamake kwa sauti moja.
Mama yake Heri kwa upole na hekima alilielezea lengo lake la kufika pale.
“Loh!” Alisema mama mwenye nyumba kwa kejeli na beuo, akauweka mtandio wake vizuri kisha akaendelea. “Hivi wewe mama una akili? Mulipotoka kwenu muliiangalia hali yenu. Mulijitizama kwenye kioo kweli? Mwanangu Rukia aolewe na kinyangarika kama huyu? Ulisema eti unafanya kazi gani vile. Eti umeajiriwa kusaidia kuuza bidhaa markiti. Si wewe niliyekuona juzi Markiti unakaa kama chokoraa? ”
Maneno hayo yaliingia katika moyo wa Heri kama kisu kilichonolewa. Moyo wake ulikatika katika na kuchuruzika damu. Mama yake naye aliumia vile vile lakini alijikaza na kutakalamu kwa ustaarabu kama kawaida yake. “Lakini mwanamke mwenzangu kumbuka sote tumeumbwa na Mungu na sote ni sawa, si vyema kubaguana na mtume rehma na amani zimshukie ametwambia kuwa mambo yanayofaa kupembelezwa katika kuchagua mume ni dini na tabia. ”
“Munakuja kwangu kisha munaanza kunifunza dini eh? Munadhani mie dini siifahamu?”
Heri mori ulimpanda na hapo hapo akainuka na kumshika mama yake mkono kisha akasema kwa ghadhabu,
“Mama tuondoke!”

Hakika lilikuwa tukio zito sana katika maisha ya Heri. Ndoto yake ya kumuoa Rukia haikuzimika tu bali pia wingu la huzuni lilimtawala kwa mabezo alioyapokea kutokana na hali yake ya ukata. Hamu ya kuoa iliyeyuka na kupotea kusikojulikana kama vuke angani. Mama yake naye aliumia vile vile kumuona mwanawe akiwa katika hali ya huzuni siku nenda siku rudi.
“Heri unamkumbuka Nasra, mtoto wa aunty Ramla?” Aliuliza mamake Heri siku moja walipokuwa wakila chajio.
“Wale waliokuwa majirani zetu tulipokuwa tukiishi Kongowea?”
“Haswaa! Unamkumbuka Nasra vyema mulivyosoma madrasa pamoja mulipokuwa wadogo?”
“Ndiyo mama. Wamepatikana na nini.”
“Wapo salama alhamdulilah. Jana niliwasiliana na Ramla na wazo la wewe kumuoa Nasra likanijia lakini bado sijamuelezea.”
“Mama jamani! Unadhani watakubali kweli?”
“Nina imani Ramla atakubali. Ni rafiki yangu wa muda mrefu na ni mwanamke mcha Mungu sana, sidhani kama hali ya mtu ya maisha inaweza ikawa pingamizi kwake.”
Heri aliona kuwa halikuwa jambo baya na jambo la muhimu ni kujitahidi kisha mengine ni kumuachia Mungu.

Siku iliyofuata mama yake Heri alifunga safari na kuelekea Kongowea kwa kina Nasra. Alipokewa vyema na Ramla alifurahi sana kumuona rafiki yake ambaye kuonana ilikuwa nadra kutokana na mihangaiko ya kimaisha. Baada ya salamu na mazungumzo marefu ya mtu na swahibaye, mama yake Heri aliamua kuelezea lengo hasa la ujio wake. Ramla alifurahi sana na hapo hapo akamuita mwanawe Nasra.
“Mama Nasra anaswali dhuha. Akimaliza ntamwambia aje.” Alijibu dada yake Nasra mdogo.
Baada ya kuswali dhuha kama kawaida yake, Nasra alienda hadi sebuleni. Kwa heshima kuu alimsalimia mgeni.
“Nasra si unamkumbuka huyu mamake Heri?”
“Namkumbuka sana mama.”
Mazungumzo yalipamba tena moto naye Nasra akakubali kuolewa na Heri. Furaha ilitawala na mikakati ya harusi ikaanza. Hatimaye Heri alimuoa Nasra na kufungua ukurasa mpya wa maisha.

Ndoa ya Heri na Nasra ilikuwa ndoa ya kupendeza iliyojaa mapenzi na itifaki. Huluka zao ziliendana vyema hivyo basi kuzidi kudumisha uhusiano na tangamano lao. Nasra alikuwa binti mwenye dini na tabia ya kupigiwa mfano kama Heri alivyokuwa. Walihimizana mambo ya heri na kuishi katika misingi mizuri ya dini. Wakati mwengine machozi yalimtoka Heri kila alipomuangalia mke wake. Alijihisi mwenye bahati kumpata mke mwenye sifa ambazo kila mume angelizitamani ziwepo kwa mkewe. Miaka miwili ilipita na wakaruzukiwa mtoto wa kike. Aidha mambo ya Heri yalianza kumfungukia na akaweza kufungua biashara yake mwenyewe.Naam,maisha yake yalinawiri na hali yake ya kifedha ilikuwa na afadhali kuliko ya awali.

Siku moja Heri na Nasra walipokuwa wakitizama runinga, Heri alistaajabishwa na kile alichokiona. Alifuta macho yake ili kuthibitisha kuwa hayamchezi shere.
“Yule si Rukia?” Aliuliza kwa mshangao mkubwa.
“Kwani unamfahamu?”
“Ndiyo namfahamu.”
Rukia na mama yake walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la kuwa walanguzi wakuu wa dawa za kulevya. Machozi yalimtiririka Heri akamkumbatia mke wake na kusema, “Namshukuru sana Mungu kwa kunipa mke wa Heri. Ama kwa hakika unaweza ukataka kitu kwa pupa na kumbe si heri na ukachukia kitu na kumbe ndio heri yako.”

2 thoughts on “MKE WA HERI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *