Ameamka mapema, ‘mekatiza usingizi
Tayari nazi kukama, na kuzibandika mbazi
Hata kama ana homa, yabidi kufanya kazi
Ni juhudi zake mama, ili mwana ubarizi
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Moto unajiwakia, nusura mtu kuchoma
Yabidi kukurubia, ili kupikike vyema
Yote anavumilia, masikini huyu mama
Nawe unashuhudia, iweje huna huruma?
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Mbio zote anakwenda, ili upate elimu
Vilivyo anajipinda, kwa kuwa na yako hamu
Kilo kumi anakanda, uone maisha tamu
Anafikia kukonda, kwa kufanya kazi ngumu
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Unapelekwa chuoni, kwa za shida darahima
Anajinyima gauni, ili ukasome vyema
Wajifanya huyaoni, unampuuza mama
Na makundi ya kihuni, vilivyo wayagandama
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Mama ana tumaini, masomo utayashika
Ili siku za usoni, usije kuhangaika
Naye awe furahani, mwangaza kummulika
Ila we u taabani, maovu ‘mejipachika
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Ulevi unatumia, si pombe si heroini
Darasani ‘mekimbia, unafuata wendani
Unaushika mkia, ufikapo mtihani
Huwezi muhurumia, mama yako masikini?
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Mimba unajishikia, mimba kabla ya ndoa
Na bila kufikiria, unaenda kuzitoa
Unajihatarishia, dada basi hili jua
Na pia mola jalia, unamuasi tambua
Kabla kujiharibia, tumfikirie mama!
Lapendeza kilisoma
Shukran