VIWAKILISHI
Viwakilishi ni maneno yanayotumika badala ya nomino(vibadala vya nomino). Nomino husika huwa haitajwi katika sentensi. Kwa mfano, yule ni mtunzi mbuji wa mashairi.
AINA ZA VIWAKILISHI
1.VIWAKILISHI NAFSI: Hivi ni viwakilishi vinavyosimamia viumbe vyenye uhai na hutokea ima katika nafsi ya kwanza, nafsi ya pili au nafsi ya tatu. Kwa mfano:
- Mimi ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Masinde Muliro
- Wewe ni mama bora.
- Yeye ni ghulamu mtanashati.
Kuna aina mbili kuu ya viwakilishi vya nafsi.
1.Viwakilishi nafsi huru: Hivi ni viwakilishi visivyohitaji kuongezewa viambishi vyovyote ili kujikamilisha. Navyo ni; mimi, sisi, wewe, nyinyi, yeye, wao.
2.Viwakilishi nafsi viambata (vitegemezi): Hivi ni viwakilishi vinavyotokea kama viambishi. Si maneno huru. Kwa mfano;
- Nilikula chapati tamu sana .
- Anatarajiwa kufika leo.
2. VIWAKILISHI VYA NGELI: Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha kuwa nomino inayohusika imo katika ngeli flani. Kwa mfano:
- Kilichopikwa ni chetu sote.
- Yatafungwa jioni.
3.VIWAKILISHI VYA SIFA: Haya ni maneno ya sifa yanayosimamia nomino. Kwa mfano, Wakubwa wasubiri wadogo wale.
4.VIWAKILISHI VYA A-UNGANIFU: Viwakilishi hivi hushirikisha majina mawili yenye uhusiano na hujengwa kwa kutumia A-unganifu. Kwa mfano, Wa zizini atachinjwa kesho.
5.VIWAKILISHI VYA PEKEE: Haya ni maneno yalioundwa kutokana na mzizi ‘-ingine’, ‘-ote’, ‘-o-ote’, ‘-enyewe’ na ‘-enye’ na kutumika kama viwakilishi. Kwa mfano:
- Lolote linakubalika.
- Wenyewe waliingia nyumbani.
- Mwenye kipaji cha kutunga mashairi amezawadiwa.
6. VIWAKILISHI VIREJESHI: Viwakilishi vinavyoundwa kutokana na kiambishi ‘o-rejeshi‘ au amba-. Kwa mfano:
- Wanaokula ni wanangu
- Nguo ambayo ulinipa ilinitosha sawa sawa.
7. VIWAKILISHI VISISITIZI: Hivi ni viwakilishi vinavyotumika kusisitiza nomino ambayo yenyewe haitajwi katika sentensi. Kwa mfano, Mwalimu anatumia Kiki hiki.
8.VIWAKILISHI VIMILIKISHI: Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha umilikaji. Kwa mfano, Chake kimepotea.
9. VIWAKILISHI VIULIZI: Viwakilishi hivi hutumika katika swali. Kwa mfano, Nani ameenda sokoni?
10. VIWAKILISHI VYA IDADI: Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha idadi. Kwa mfano, Vinne vinatosha.
11.VIWAKILISHI VIONYESHI(VIASHIRIA): Hivi ni viwakilishi vinavyoashiria kitu kinachozungumziwa. Kwa mfano, Yule alinisaidia sana.
MAREJELEO
- Kimani Njogu na Dorothy K. Nganje, kiswahili kwa vyuo vya ualimu: Jomo Kenyatta Foundation 2006.
- Kimani Njogu, Alice Mwihaki na Aswani Buliba, Sarufi ya kiswahili: uchanganuzi na matumizi: Jomo Kenyatta Foundation 2006.
- G. Waihiga na K.W. Wamitila, chemichemi za kiswahili kidato cha pili 2003
ASANTE SANA
Karibu
aki thanks so much this has helped me with my swahili homework
Nimefurahi umesaidika