VIUNGANISHI
Viunganishi ni maneno yanayotumiwa kuunganisha vipashio mbali mbali vya lugha. Kwa kawaida, huunganisha vipashio vifuatavyo:
- Neno na neno
- Kirai na kirai
- Kishazi na kishazi
- Sentensi na sentensi
AINA ZA VIUNGANISHI
1. VIUNGANISHI VYA SABABU: Viunganishi hivi huunganisha hali moja na sababu yake. Kwa mfano, aliadhibiwa kwa sababu alichelewa.
2.VIUNGANISHI VYA MASHARTI: Viunganishi hivi huunganisha hali na masharti ya hali hiyo. Kwa mfano, iwapo atamaliza mitihani mapema, ataenda kwa shangazi yake.
3. VIUNGANISHI VYA TOFAUTI: Viunganishi hivi huonyesha tofauti baina ya kitu/hali moja na nyingine. Kwa mfano, wanafunzi wote wamefaulu mtihani isipokuwa wanafunzi wawili.
4. VIUNGANISHI VYA KUTEUA: Hivi hudhihirisha uchaguzi au uteuzi baina ya vitu viwili au zaidi. Kwa mfano, utaenda Malindi au Lamu?
5. VIUNGANISHI VYA ZIADA: Hivi huonyesha hali au vitu vya ziada, licha ya vile vilivyotajwa mwanzo. Kwa mfano, na, pia, aidha, licha, pamoja na.
Mifano katika sentensi:
- Alikula chapati, viazi vya nazi na sambusa.
- Licha ya kuwa mwanauchumi, ni mwandishi.
6. VIUNGANISHI VILINGANISHI: Hivi hulinganisha vitu viwili au zaidi. Kwa mfano: Sembuse, kuliko, zaidi ya, seuze.
Mifano katika sentensi:
- Anapenda chapati kuliko wali.
- Umeshindwa kuamka saa moja asubuhi, seuzi saa kumi alfajiri?
MAREJELEO
- Kimani Njogu na Dorothy K. Nganje, kiswahili kwa vyuo vya ualimu: Jomo Kenyatta Foundation 2006