PEPO! MASKANI YA DAIMA

      No Comments on PEPO! MASKANI YA DAIMA

Kalamu niishishie, natunga toka moyoni
Dua zetu tukidhie, twakuomba ya manani
Motoni usitutie, adhabu hatuwezani
Ewe mola tujalie, pepo iwe masikani

Tujaalie ni wema, tutende mambo ya kheri
Tutende bila kukoma, tena kwa hamu na ari
Ili tupate salama, tukae mbali na nari
Pepo nyumba ya daima, tujalie ya Qahari

Tuwe ni wenye kutubu, pindi tunapokosea
Ya ghaffari ya wahabu, toba anazipokea
Wala tusione tabu, kwa mola kuelekea
Tutaepuka adhabu, na peponi kuingia

Hakika hini dunia, si baiti ya daima
Sote ni wapita njia, hilo tukumbuke vyema
Hakuna atobakia, mola amekwishasema
Yaa rabbi twakulilia, tujalie pepo njema

Isitughuri dunia, kwa mapambo ainati
Dini tukaikimbia, vishawishi vingi eti
Mwishowe tusije lia, tukabaki na laiti
Nyumba ya kukimbilia, si nyingine ni janati

Lolote tunalotenda, tufanye kwa moja nia
Ni iwe tutajipinda, kumridhisha jalia
Hapo mola ‘tatupenda, adhabu kutwepushia
Na daraja tutapanda, jannati kuingia

‘Situshughulishe sana, harakati za dunia
Shughuli zikatubana, kheri kutojifanyia
Amri zake rabana, tukazipuuzilia
Tuweni makini sana, pepo kuikimbilia

Pepo nyumba ilo aali, ya milele masikani
Kuna mito ya asali, nao pia hurulaini
Hini dunia kwa kweli, si ya daima jamani
Tufanyeni kila hali, hatima iwe peponi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *