KUDHIBITI MUDA

      No Comments on KUDHIBITI MUDA

Muda ni kitu muhimu katika maisha ya binadamu yeyote yule. Kizuri zaidi ni kuwa huu muda tumeubeba sisi wenyewe na tuna uhuru wa kuendesha tunavyotaka; ima tuutumie kuotesha matunda au tuupoteze. Katika hii dunia wapo watu aina mbili; wale waliofanikiwa au wapo katika mchakato wa kufanikiwa na wale ambao kwamba wapo mbali na mafanikio. Hivi ni kwa nini kuwepo tofauti hii wakati sote tuna masaa ishirini na manne katika siku? Naam, bila shaka ni udhibiti wa muda. Tuelewane vyema, udhibiti mzuri wa muda sio jambo pekee linalochangia kuleta mafanikio lakini ni sababu aula miongoni mwa msururu wa sababu nyenginezo. Wapo wanaofahamu kuwa muda upo na unatosha kufanikisha yote yaliomo kwenye ratiba zao, kinachotakiwa ni kuudhibiti muda huo vyema. Wapo pia ambao daima wanaona muda hautoshi, hivyo basi hawawezi kufanikisha au kutimiza ndoto zao. Bila shaka hiyo ni fikra finyu isiokuwa na ukweli wowote ndani yake. Ni wangapi wanasoma huku wakifanya kazi ya kujipatia kipato na wakapata alama nzuri zaidi kuliko wale waliowekeza muda wao wote kwenye masomo? Muda ukitumika ipasavyo basi mambo aina ainati yanaweza kutimizwa ndani ya muda mchache.

Kama sote tunavyofahamu, jani likipukutika kutoka kwenye mti basi kurudi tena ni muhali. Hivyo ndivyo ulivyo muda. Muda ukishapita haurudi tena.
“Natamani ningeweza kuurudisha muda nyuma.” Haya ni maneno ambayo kwamba wengi tumeyasikia kutoka kwenye vinywa vya wale waliozama kwenye majuto kwa kuutumia muda wao vibaya. Au pengine sisi wenyewe tulishawahi yatamka maneno mfano na hayo. Mafunzo ya dini vile vile yametilia mkazo masuala ya muda. Kwa mfano, katika imani ya kiislamu, mtu anapokufa huwa anatamani apewe lau muda mchache ili aje afanye amali njema. Hivyo basi, ni muhimu kuhakikisha kuwa unaitumia kila sekunde kuongeza thamani katika maisha yako. Ule muda unaoupoteza kufanya mambo yasiokuwa na manufaa yeyote katika maisha yako unaweza ukautumia ukaleta mabadiliko makubwa kwako iwapo tu utauthamini.

Je una malengo au ndoto zaidi ya moja, na unataka kuzitimiza zote kwasababu unaziona zote ni muhimu? Bila shaka watu huenda wakakwambia hilo jambo haliwezekani na ni vyema kufanya jambo moja tu. Mmh! Pengine sababu yao kuu ni nini? Muda! Kama sababu ni muda basi suluhisho la kudumu lipo. Wakati tunao mwingi sana lakini jinsi tunavyoutumia kunatufanya tujione daima tuko mbioni na wakati huo haututoshi. Kitu muhimu tunachopaswa kufahamu ni kuwa udhibiti wa muda unafaa kuwa sehemu ya maisha yetu.

Yafuatayo ni mambo ambayo nina imani yatakusaidia katika kuudhibiti muda wako na kutimiza ndoto zako zote bila muda kuwa kikwazo.

1) YAFAHAMU MALENGO 

Miongoni mwa mambo muhimu katika suala zima la kudhibiti muda ni mtu kufahamu malengo yake anayotaka kutimiza. Haiyamkiniki mtu kukurupuka na kuanza kufanya jambo flani bila kufahamu hasa anafanya kitu gani au ni ipi hatma ya kile anachokifanya.Iwapo utafanya  hivyo, basi huenda  ukapoteza muda  mwingi  sana kufikiria kila siku ni kitu gani unataka  kufanikisha. Hivyo  basi, ni vyema kuyaandika chini malengo yako yote. Hili litakusaidia kuyakumbuka yale yote unayotaka kuyatimiza na yanapaswa kutimizwa kwa muda gani. Kwa mfano, ikiwa unataka kuchapisha kitabu mwaka 2020, basi ni vyema kuandika hilo chini na pia kuliweka akilini. Hii itakusaidia kujipanga vyema na kufahamu ni kwa muda gani utaandika kitabu chako na pia muda wote ambao mchakato mzima wa uchapishaji utachukua. Hili linatupeleka katika hoja yetu ya pili, KUJIPANGA VYEMA

2) JIPANGE VYEMA

Nakumbuka nilipokuwa shuleni walimu walikuwa wakitusisitizia sana kuhusu nidhamu (self discipline).Naam, nimekuja kuamini kuwa,  kuwa na nidhamu  ni jambo muhimu katika maisha na pia ni kichocheo cha mafanikio. Ukijipanga vyema basi huenda ukafanikisha mambo mengi ndani ya muda mchache. Zipo njia nyingi unazoweza kutumia ili kuhakikisha mambo yanaenda kwa mpangilio mzuri . Kwanza kabisa,  unaweza ukaandika ratiba itakayokuelekeza ni jambo gani unapaswa kufanya wakati gani na kwa muda gani. Katika kuandika ratiba yako, ni jambo la busara kuyapa kipaumbele yale mambo unayoyaona muhimu zaidi. Unaweza ukayaweka mambo hayo muhimu katika masaa ya kwanza ya siku, yaani alfajiri wakati ambapo akili bado haijachoshwa na shughuli za siku. Au pia kama  huna ratiba unaweza ukatumia dakika takriban ishirini baada ya kuamka kuandika matukio yote unayotaka kufanya siku hiyo. Hili litakusaidia kutopoteza muda baadae katika siku kufikiria ni kitu gani ufanye na kwa wakati gani. Aidha, ni vyema kujipanga kulala mapema ili siku itakayofuata uamke mapema ukiwa mwingi wa uchangamfu na kuanza shughuli zako mapema. Bila shaka ukianza mambo yako mapema utakuta muda upo mwingi wa kutimiza mambo yote ya siku hiyo.

3)ANDAA AU NENDA KWENYE MAZINGIRA AU MANDHARI UNAYOYAONA BORA KWAKO KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZAKO

Mapenzi ya mazingira flani yanatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwengine. Wengine wanapenda kutekeleza shughuli zao sehemu ilio kimya na tulivu na pia wapo wanaopenda sehemu iliochangamka kidogo. Hivyo basi, ni vyema kujiandalia mazingira ambayo yatakusaidia kufanya kazi zako vizuri zaidi. Unaweza ukaandaa chumba chako vizuri na kuamua kuwa itakuwa sehemu yako ya kazi. Kwa mfano  kama ni msomi au mwandishi, unaweza ukaandaa meza, ukapanga vitabu, ukaweka maua, ukabandika maneno yenye hamasa kwenye ukuta na kuyaandika malengo yako vyema pia ukayabandika ukutani. Au wengine wanapenda kusoma au kuandika wakiwa kwenye maktaba au hata baharini huku wakiangalia mawimbi ya bahari na upepo ukiwavumia. Hili linasaidia akili kufanya kazi vizuri zaidi, hivyo basi ukamaliza shughuli zako ndani ya muda mchache.

4) ONDOSHA VITU VYENYE KUKUTAGHAFALISHA

Dunia yetu ya sasa kumejaa vitu ambavyo kwamba mara moja vinaweza kuibadilisha akili yako na  kuitoa kwenye jambo moja na kuipeleka kwenye jambo jingine. Kwa mfano, simu au runinga. Ni vyema, unapokuwa katika harakati ya kutekeleza kazi yako kuondosha vitu kama hivyo. Kwa mfano, unaweza ukawa umezama ji katika kazi flani mara ukaamua kushika simu kwa dakika chache ili uingie katika mitandao ya kijamii. Utaangalia labda video na hamu itakuzidia utaangalia ya pili na ya tatu mpaka ukitahamaki muda umesonga sana. Hili linaweza kukusababishia kutomakinika katika kufanya kazi,hivyo basi kuchukua muda mwingi katika kazi moja.

5) JISHUGHULISHE KILA UNAPOPATA WAKATI 

Kuna muda unaoupata sehemu flani ambao kwamba unaweza ukautumia vizuri sana badala ya kuupoteza kiholela. Kwa mfano, ukiwa kwenye  foleni benki unaweza ukaendelea kusoma riwaya yako au ukatunga shairi. Ukiwa kwenye gari hali kadhalika unaweza ukamalizia kuhariri video unayotaka kutuma YouTube. Al hasili kila muda unaoupata utumie vyema na hili litakusaidia kutekeleza yale yote unayodhamiria kufanikisha.

6) KATAA MAOMBI 

Naam, ni vigumu sana kwa watu wengine kusema neno hapana hasa kwa wapendwa wao kwasababu wanahofia kuwaumiza. Bila shaka ni vyema kuwepo wapendwa wako wanapokuhitajia lakini pia si vibaya kukataa baadhi ya maombi ambayo kwamba hayana umuhimu wa kivile. Unapokuwa katika shughuli zako ambazo ulikuwa umezipangia kuisha siku hiyo alafu rafiki yako akuombe umpeleke matembezi labda, basi una uhuru kukataa ombi hilo kwa upole na umueleze kuwa kuna shughuli unamalizia. Ikiwa utakubali kwenda kila sehemu au kufanya kila unaloagizwa (yasio ya muhimu) basi huenda ukapoteza muda mwingi sana na ukashindwa kufanikisha malengo yako.

7) USIAHIRISHE

Hakuna adui mkubwa wa mafanikio kama uahirishaji. Unapoamua kufanya jambo flani basi hakikisha unalifanya mpaka unalimaliza ndani ya muda uliouandaa. Kuahirisha kutakupelekea kutomaliza au kufanya jambo moja kwa muda mrefu kuliko maelezo.

8) JIHAMASISHE

Ninachoamini ni kuwa hamasa ni muhimu katika safari ya mafanikio. Kama binadamu, tunahitaji kuhamasishwa ili tupate msukumo wa kufanya mambo zaidi na zaidi. Unaweza ukaamka asubuhi ukataka kutekeleza yale yote ulioyaandaa Siku hiyo lakini ukajihisi huna hamu. Hivyo basi, ni muhimu kujihamasisha kwa kutizama video za kuhamasisha, kujizawadi au pia kwa kujikumbusha sababu ya wewe kutaka kutekeleza ndoto zako. Hili litakusaidia kufanya yote unayodhamiria kufanya bila kupoteza muda kwa kutoyafanya.

9) BADILISHA RATIBA 

Bila shaka unapoona kuwa kumuekea panya sumu kwenye chakula haisaidii basi mtegee mtego.Ikiwa utaona mbinu au ratiba unayotumia haikusaidii basi unaweza ukatumia mbinu tofauti ambayo unahisi itakusaidia kuhifadhi muda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *