BINTI NIMPELEKE CHUO KIKUU?

      No Comments on BINTI NIMPELEKE CHUO KIKUU?

Kithwa sana nimekuna, mpaka  hunihairi
Mawazo ‘mesongamana, mawazo yalo kathiri
Nijibuni waungwana, uniishe utiriri
Msichana wangu mwana, nimpeleke chuoni?

Visa vilo vingi sana, hakika ‘mevisikia
‘Mepotea wasichana, chuoni waliongia
Moyo hunipiga sana, kila nikifikiria
Binti yangu waungwana, nimpeleke chuoni?

‘Limsikia zenabu, kutoka mwake kinywani
Binti yake muhibu, na la jicho lake mboni
Habanduki maklabu, nguo zake ni vimini
Mie bado nisitubu, binti aende chuoni?

Jirani yangu sofia, hana raha asilani
Habari ‘mezisikia, za mwanawe wa chuoni
Mimba amejiavyia, hali yake taabani
Na mimi mwanangu pia, nimpeleke chuoni?

‘Linieleza sakina, na tena huku alia
‘Mepotea wake mwana, tangu chuoni kungia
Hijabu havai tena, swala amezikimbia
Nisikome wangu mwana, nimpeleke chuoni?

Lakini naye halima, alipelekwa chuoni
Akamaliza salama, salama wa salmini
‘Metunza yake heshima, nayo pia yake dini
Na mwanangu naye jama, nimpeleke chuoni?

‘Mechanganyikiwa sana, akili ‘mekorogeka
Nahofia wangu mwana, asije kuharibika
Uso wangu waungwana, ni wapi nitauweka?
Alo wa pekee mwana, nimpeleke chuoni?

Malezi yalo ya dini, binti yangu nimempa
Ametia akilini, ila bado naogopa
Wapo wengi fahamuni, ‘lofunzwa waliyatupa
Binti yangu jamani, nimpeleke chuoni?

Wapo waliolelewa, malezi yalio mema
Na dini walifundishwa, wakawa ni waja wema
Lakini kulipokuchwa, shetani ‘kawagandama
Mtoto wangu kesho kutwa, nimpeleke chuoni?

Suluhisho naamini, lipo tena lipo sana
Tukesha mfunza dini, tumueke chini nana
Tumwambie kiundani, yale tusosemezana
Yamwingie akilini, kisha aende chuoni

Na jambo lilo muhimu, ni kuwaombea dua
Uongofu tufahamu, Mola ndio anotoa
In shaa Allah mola rahimu, wana ‘tatuongozea
Daima ‘tajiheshimu, pia wakiwa chuoni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *