
Ndugu nawasimulia, kwa mengi mno machungu
Mimi yalonifikia, ninajuta wenzi wangu
Nasema huku nalia, dunia naona chungu
Yameniharibikia, jamani maisha yangu
Nilifaulu vizuri, huko shule ya upili
Mama kaona fahari, akafurahika kweli
Ilitujaa sururi, tukashukuru jalali
Tukajua ni safari, ya sisi kufika mbali
Dada yangu kadhalika, mtihani alipasi
Naye alifurahika, ikaburudi nafusi
Mama ahadi kaweka, chuo tutaenda sisi
Hata kama ni kupika, na kuziuza juisi
Hatimaye tulienda, katika chuo sifika
Mno si tulijipinda, na masomo kuyashika
Walimu walitupenda, kwa njema zetu huluka
Tulikuwa chema chanda, na pete wakatuvika
Niliianza tabia, ya kuenda vilabuni
Akili ilinambia, sitofanya ya kihuni
Najua nimekulia, kwenye malezi ya dini
Kumbe shetani sikia, huanza namna hini
Nikawapata wendani, maovu matendo yao
Vitimbi vya chini chini, wakanifanyia wao
Hatimaye masikini, ‘kaingilia vileo
Mafundisho ya kidini, nikayapatia ndweo
Kwa pombe nilianzia, haitoshi nikaona
Unga nikaingilia, vileo vya kila namna
Wendani wakanambia, onja bangi utaona
Mi bila kufikiria, nikajitosa kwa kina
Nikawa sijifahamu, ulevini nimezama
Masomo yakawa sumu, sitaki tena kusoma
Ikanizidia hamu, ulevi bila kukoma
Zikanipanda stimu,nikawa tena si mwema
Zikawa hazinitoshi, pesa anotuma mama
Vikazidi vishawishi, ulevini nimezama
Siezi tena kuishi, bila ya bangi kuchoma
‘Meharibika aushi, imepotea salama
Maradhi ‘kasingizia, ili nitumiwe hela
Mama ananitumia, japo kwa mingi madhila
Ugumu avumilia, wa kuzitafuta hela
Bila kumfikiria ,nazifanya nyingi hila
Dadangu kipenzi pia, na yeye sikumsaza
Ulevini kamtia, naye kaanza kuoza
Ulevi akatumia, akiliye ikapoza
Madawa yakamuingia, hakuweza kujikaza
Pesa tukazimaliza, haikubaki sumni
Na dawa tukizisaza,tunakuwa taabani
Nikaanza kumuuza, dadangu bila imani
Ili tu kutosheleza, mambo yetu ya kihuni
Tulifukuzwa mwishowe, katika chuo kikuu
Kilimshika kiwewe, mama kuona makuu
Kwa kuwaona wanawe, kupata mkasa huu
Bidii zake za mwewe, leo amekula huu
Masikitiko kwa kweli, mama yalimuingia
Kuziona zetu hali, alibaki akilia
Kisu chenye ncha kali, moyoni kilimuingia
Aliyaona shubili, maisha ya hii dunia
Majuto ni mjukuu, kwa kweli nimeamini
‘Sosikia la mkuu, wala asilithamini
Huvunjika lake guu, akabaki hasarani
Maovu yalo makuu, yakawa wake mwendani
Ninawapa ushauri, enyi vijana wenzangu
Abadani ‘siwaghuri, maisha ya kilimwengu
Madawa sio mazuri, madhara yake machungu
Basi ishini vizuri, ‘siwafike kama yangu
Mashallah kipaji kizuri mama. Una mtiririko Mzuri na Visa vizuri . Nadhimiria kukuona ukiandika hadithi fupi na tamthilia. Kila la kheir
Asante sana