JINSI YA KUPIKA MAHAMRI YA NAZI YA USWAHILINI

Licha ya mahamri kuwa chakula rahisi kupika pia ni chakula kinachohitaji mahitaji ya kawaida sana yanayopatikana Katika duka au soko lolote lile. Aidha ni chakula maarufu na kinachopendwa na wengi hasa katika kanda ya pwani. Mbaazi nazo tunaweza kuziita ndugu yake mahamri kwani ni vyakula viwili vinavyoendana sambamba. Ni nadra sana upite katika mitaa ya uswahilini ukose mama aliyekaa nje na karai akipika mahamri au mbaazi .Naam, na hii ndiyo raha ya pwani. Wakati wowote ukisikia njaa ni rahisi sana kupata chakula mtaani.

MAHITAJI 

 • Vikombe 4 vya unga wa ngano
 • Mafuta ya kupikia vijiko 2 vya mezani
 • Glasi 1 ya maji(unaweza ukatumia tui glass 1 badala ya maji kama huna nazi ya unga)
 • Nazi ya unga vijiko 6 vya mezani
 • Iliki kijiko 1 kidogo
 • Hamira kijiko 1 kikubwa
 • Sukari vijiko 6

MATAYARISHO

 • Tengeneza shimo kwenye unga ueke mahitaji yote isipokuwa maji. Kisha weka maji kidogo uchanganye mpaka sukari iyeyuke.

 • Sukari ikishayeyuka endelea kueka maji huku ukichanganya unga wote. Changanya mpaka unga ushikane. Hakikisha unga hauwi laini sana wala mgumu sana, uwe wastani. Endelea kukanda unga wako kwa takriban dakika kumi hivi.

 • Funika unga wako uuache kwa takriban dakika 10. Kisha tengeza madonge madogo madogo. Kwa kiasi hiki cha unga nimepata madonge 5 na donge moja dogo. Au pia unaweza ukatengeza madonge madogo madogo sana ili utengeze mahamri ya duara.

 • Funika madonge yako uyaache kwa takriban saa 1 yaumuke. Ikiwa uko sehemu ya baridi au una haraka, washa oven kwa takriban dakika 5,izime kisha weka madonge yako ndani ili ule mvuke usaidie mahamri kuumuka.

 • Madonge yashaumuka hapo. Sukuma donge moja moja ukate mara 4 liwe shape ya pembe tatu.

 • Bandika mafuta ya kupikia motoni na yakishika moto weka mahamri uanze kuyakaanga(hakikisha mafuta yanashika moto vizuri ili mahamri yafure vizuri yakiwa motoni lakini pia yasishike moto kupita kiasi mahamri yakaungua) mahamri yakishashika rangi nzuri ya hudhurungi geuza upande wa pili ili nao pia ushike rangi nzuri ya hudhurungi. Yatoe mahamri kwenye mafuta uyaweke kwenye bakuli la kuchuja mafuta. Na mahamri yako yapo tayari.

 • Andaa kwa chai aina yeyote, mbaazi au hata maini.

KWA MAPISHI ZAIDI UTANIPATA

 • YOUTUBE @farwat’s kitchen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *