HULKA YA DHAHABU _UKARIMU

      2 Comments on HULKA YA DHAHABU _UKARIMU

Ukarimu ni huluka, inayoleta furaha
Fuadi hunawirika, zikayeyuka karaha
Na lengine kadhalika,huyapoza majeraha

Ndugu tuwe wakarimu, popote tukitokea
Kwa watu tutabasamu,na mema kuwatendea
Maisha ‘takuwa tamu,na furaha kuenea

Ukarimu ni huluka adhwimu inayoyeyusha nyoyo  nyweee kama aiskirimu ya vanilla. Vile vile, ukarimu ni lugha  inayofahamika na watu wa aina zote ulimwenguni,  si mwana mchanga, si kikongwe, si kiziwi,  si kipofu. Aidha ni tabia inayootesha miti ya furaha hata katika nyoyo zilizokata tamaa na kulizika neno furaha katika shimo lenye kina kirefu. Ukarimu una nguvu za ajabu zinazoweza kuubadilisha moyo mweusi ti na kufanya uwe mweupe kuliko pamba. Zile chembe chembe za ukarimu unazoziacha katika moyo wa mtu na kuziona ndogo kuliko sisimizi, huenda zikachipuka na kukita mizizi ya daima katika moyo wa mtu huyo. Naam, wapo wengi kwao ukarimu ni kama kunywa maji, yaani ni tabia ambayo kwamba imekuwa mfumo wa maisha yao. Kwa upande mwingine, wapo wale ambao kwamba ukarimu kwao ni jambo adimu na hutokea kwa nadra sana katika maisha yao. Tukiangalia kwa umakini na uangalifu zaidi, tutagundua kuwa ile aina ya kwanza ndiyo watu wenye furaha kuliko aina hii ya pili. Ni dhahiri kuwa kadri unavyoeneza furaha kwa watu wengine ndivyo inavyozidi furaha yako. Abaadan hawakukosea wale waliokuli kuwa ukitaka kuwa na furaha basi wafurahishe wengine.

Kuwa mkarimu haigharimu chochote na wala haipunguzi chochote katika maisha ya mtu bali humzidishia furaha. Hivyo basi,ni kwa nini tusilivae vazi la ukarimu na kulifanya liwe vazi letu la daima? Ni kwa nini tusizigeuze nyoyo zetu zilizojaa chuki, tamaa na vinyongo kuwa nyoyo zilizotawaliwa na ukarimu? Ni kwa nini tusizioshe nyoyo zetu kutumia maji ya dhahabu na kuziachia japo athari au matone ya maji hayo? Waama, ukarimu haimaanishi kuwasaidia watu kwa kutumia mamilioni ya pesa. La! Kukutana na mtu njiani ima unayemfahamu au usiyemfahamu na kumsalimia huku ukitabasamu ni ukarimu tosha. Ukifanya hivyo, bila shaka utahisi upepo mwanana wa furaha ukivuma ndani ya moyo wako. Naye akirejesha salamu na tabasamu utahisi kama kuna uhusiano flani baina yenu japo ni ajinabii. Vuta hii picha, unatembea njiani kisha ukutane na mtu flani uamue kumsalimia kwa kumshashia na kumtabasamia na akujibu huku sura kaikunja kama aliyeramba ndimu, utahisi vipi katika moyo wako? Kwanza maswali mingi yataitawala akili yako. ‘Kwani nimemkosea? Nimemtendea nini jamani? Mbona ameninunia?’ Licha ya hayo,huenda hata ukajuta kumsalimia. Vivyo hivyo ndivyo mwengine atahisi iwapo utamfanyia kama hivyo.

Unadhani ni furaha iliyoje itakayokutawala iwapo utawaona watu wakiwa wenye furaha na wewe ndio chanzo? Au watu wakishusha pumzi na kuhisi afueni kwa kuwashushia mzigo mzito waliokuwa wameubeba katika maisha yao? Bila shaka ni furaha kuu itakayokutawala. Naam, ni jambo la kuvutia na kuyeyusha moyo kumuona binadamu yeyote yule akiwa mkarimu sio tu kwa binadamu wenzake bali hata kwa wanyama. Unapotizama runinga na kumuona mtu aliyejitolea ala kulli hali kuwasimamia mayatima kwa moyo mmoja ni kitu gani kinakupitikia Katika akili na moyo wako? Bila shaka ni hisia ya kupendezwa na kitendo kile.  Hebu fikiria, furaha unayoipata kwa kumuona tu mtu akiwatendea wema wengine,je ni furaha gani utakayoipata ikiwa ni wewe unayehakikisha binadamu  wengine  wapo furahani? Hivyo basi,  jitengee siku katika wiki, mwezi au hata mwaka uende hospitalini kuwatembelea wagonjwa, uwapelekee matunda, uwajulie hali, uwakumbatie na kuwaombea dua uone watakavyofurahika na kuingiwa na matumaini. Au nenda ukatembelee kituo cha watoto mayatima uwapelekee zawadi, ucheze nao,uwakumbatie na kuwaambia maneno mazuri yatakayowafanya hata wale waliokata tamaa kuona tena mwanga. Zile tabasamu na furaha utakazoziona katika nyuso za watoto hawa niamini zitazaa matunda ya furaha katika moyo wako. Mfano mwengine ni kutembelea watu wa aila yako. Dunia yetu ya sasa shughuli zimekuwa nyingi kiasi cha kwamba muda wa kutembeleana umekuwa adimu. Wanafamilia kujumuika kwa pamoja labda iwe siku ya idi, Siku ya harusi au matanga. Usikubali asilani shughuli za kidunia zikuondolee fursa ya kuwatendea ukarimu watu wa familia yako. Jifunge kibwebwe na utenge siku moja katika wiki uwatembelee na uwapelekee zawadi japo matunda ya shilingi hamsini. Hili bila shaka litajenga mapenzi, kuzidisha udugu na kueneza furaha. Kwa wale walio mbali nawe, wapigie simu japo mara moja kwa wiki, wajulie hali na uwaulize kama wanahitaji msaada wowote kutoka kwako. Haya ni mambo ‘madogo madogo’ tunaoyadharau lakini huenda yakabadilisha maisha ya wengi na kuleta furaha ambayo kwamba kwa wengi  ni neno lililopoteza maana.

Binafsi ukarimu ni huluka inayonipendeza na kuuyeyusha moyo wangu si haba. Kipo kisa kilichonitokea ambacho abaadan kimekataa kufutika katika akili yangu. Ni takriban miaka minne imepita lakini taswira ya kisa hicho bado ipo safi katika akili yangu. Nilikuwa nimetoka sokoni na mzigo nilioubeba ulikuwa mzito sana. Kwa hakika mzigo ule ulinilemea sana kiasi cha kwamba nilitembea nikigutia. “Assalam alaikum farwa. ” Alinisalimia mtu wa kwanza ambaye kwamba tulikuwa tukifahamiana. Tulijuliana hali vizuri kisha akashika sabili na kwenda zake. “Farwa hujambo.” Alinisalimia wa pili na kushika hamsini zake. Nilikutana na marafiki zangu kadhaa na wote walinisalimia na kutokomea bila hata kujali dhiki na uzito niliokuwa nikiupata kutokana na mzigo ule. “Assalam alaikum! Naweza nikakusaidia?” Alinisalimia mvulana mdogo aliyekuwa hatufahamiani mwenye takriban miaka kumi hivi aliyekuwa akiendesha baiskeli. Nilimuitikia salamu na kumkubalia anisaidie. Kiukweli sikutaka kumuumiza kwa kumbebesha mzigo ule lakini niliiona hamu katika uso wake ya kutaka kunisaidia. Aliegesha baiskeli yake kando, akanibebea mzigo wangu na kunipandishia ngazi hadi juu kwetu. Nilipendezwa hadi ya kupendezwa na hulka ya kijana  yule. Ukarimu wake ulipenyeza ndani ya moyo wangu na kuotesha miti ya furaha ambayo katu yamekataa kunyauka hadi leo. Kila nikimkumbuka kiukweli namuombea Mungu yeye na walezi wake waliomlea vyema na kumfundisha maana halisi ya utu na ukarimu. Kitendo kile pengine yule mtoto alikiona kidogo sana na huenda hivi leo hata alikwishakisahau kitambo lakini kwangu ni jambo nililolipa thamani kubwa sana. Hivyo ndivyo ukarimu unavyoweza kumuathiri mtu. Hujui ni nani utakayemsaidia na akabaki akikuombea  Mungu milele. Bila shaka, ukarimu ni hulka ya dhahabu!

2 thoughts on “HULKA YA DHAHABU _UKARIMU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *