MAISHA KITENDAWILI

      No Comments on MAISHA KITENDAWILI

Maisha kitendawili, vigumu kuyategua
Yana na mengi maswali, kichwani yanasumbua
Tenda lile tenda hili, insi hutomtua
Ungawa mtu aali, ila bado ‘takuua

Umtendee mazuri, umlishe na kababu
Umvalishe hariri, na vidani vya dhahabu
Uzidi kutahadhari, ili usimpe tabu
Hatimaye sio siri, ‘tayafanya ya ajabu

Uishi kwa itifaki, uogope kumuudhi
Mwenyewe ujipe dhiki, ili yeye awe radhi
Tagundua habebeki, anayo mengi maudhi
Kukurushia bunduki, yeye anataaradhi

Tenda mema mia mbili, uteleze mara moja
Hawatotia akili, watakusengenya waja
‘Tasahau ya awali, wakuonyeshe vioja
Wakuone ni katili, kwa ubaya kukutaja

Nzito zao tabia, katu hawaeleweki
Lolote ‘kiwafanyia, kwao halithaminiki
Mwezi ‘ngawaangulia, ‘takuona mnafiki
Rohoni wataumia, na kujaza nyingi chuki

Ndio hali halisia, sisi ilotuzunguka
Si kote ukiingia, utaenda kupendeka
Ingawa ‘tawafanyia, mazuri ya kusifika
Wengi watakuchukia, wakuone nyangarika

Wahenga wametwambia, tenda wema nenda zako
Ikiwa watarajia, waone uzuri wako
Hakika utaumia, upate masikitiko
Ubakie ukilia, kwa kupata mshtuko

Wengi hawatothamini, yale utowafanyia
Yawe elfu milioni, watajisahaulia
Hivyo fanya kwa imani, isafishe yako nia
Malipo kwake manani,iwe utatarajia

Ishi nao wote vyema, usitaraji sawia
Tabia zisizo njema, jaribu kuvumilia
Na hata wakikusema, usibadilishe nia
Ni mafunzo ya hashima, na mwenendo wake pia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *