
Naanda kumswalia, kipendi chetu sharifu
Mtume wetu nabia, kwa furaha namsifu
Mahaba yameningia, shahidi yangu raufu
Mtukufu wa daraja, mola amemteua
Mbora wa wote waja, sote tunamtambua
Sifa zake nazitaja, ili tupate zijua
Swifa zake ni sufufu,si mbili wala si moja
Alichukia uchafu, hiyo ni ya kwanda hoja
‘lihimiza unadhifu, kwenye hadithi ‘metaja
Kwa cheo alichonacho , Mola alimtukuza
Na hakuwa na kijicho , ya watu kufwatiliza
Kidogo ajaliwacho, chali kimtosheleza
Alipenda mafakiri , na huku akiwalisha
Na mambo yalo mazuri , Tumwa ‘likiwaonyesha
Kwa kuwa ndie muniri , nuru aliipitisha
Alijali ujirani ,na vyema kuuamili
Na kwa yake ihsani ,tumwa aliukubali
Kwa maneno ya mbinguni ,Kupitia jibrili
Alipenda mayatima, kichwani ‘kiwapapasa
‘liwaonea huruma, katu hakuwanyanyasa
Basi nasi wake umma, kuwalea yatupasa
Upole yake huluka ,hakuwa mwenye ghadhabu
Kote kote ‘lisifika, wengine pia waarabu
Alimpenda rabuka , na kumuita habibu
Mtume wetu sharifu, tabia yake hariri
Alikuwa mwaminifu, ‘kiweka za watu siri
‘Limkabidhi bila hofu, hata wale makafiri
Alikichukia sana, tabia watu kuteta
Na ile ya kupigana, na kuvieneza vita
Familia kutengana, na kizazi kukikata
Sifa za wetu nabia, katu hazina mithali
Ni mbora wa dunia, kipenzi chake jalali
Sisi ametuachia, dini nzuri na aali
Mtukufu huyu bwana, kihaki tumpendeni
Tufuate zake sunna, pia tumswalieni
Ili kesho kwenye janna, tuweni naye pembeni
Hapa kikomo naweka, muda umesonga sana
Sijamaliza hakika, kumpa sifa nabina
Jina langu farshika, kwaherini waungwana
Masyaallah, beautiful photo. Can I share your this page ? regards
Maa Shaa Allah..Allah akuzidishie na vipaji
Shukran
Amiin