
Mno huvifurahia
Viswa nikivisikia
Vya waliotangulia
Ndani ‘kiwemo bilali
Ni viswa vya maswahaba
vingi na wala si haba
Na vimo kwenye vitaba
Pia katajwa bilali
Basi leo ikhiwani
Kiswa nawaelezeni
Cha wa kwanza muadhini
Si mwengine ni bilali
Na ni yupi wake mama
Si mwengine ni hammama
Kamzaa mwana mwema
Kipenzi chetu bilali
Ndugu zangu sikieni
‘limteua amini
Ili awe muadhini
Akakubali bilali
Ni Mtumwa wa awali
Kumkubali rasuli
Kamuamini jalali
Na kusilimu bilali
Imani yake thabiti
Kidini kajizatiti
Dini kangilia kati
kuinusuru bilali
Mateso ‘lipokithiri
Kutoka kwa makafiri
Alivaa ujasiri
Na kusubiri bilali
Alipokufa amini
Alishindwa kuadhini
Kwa kubwa mno huzuni
Ilomtanda bilali
Alipokufa nabina
Alihamia madina
Kwani muda mwingi sana
Alikiwaza bilali
Muda uliposongea
Kaburi kutoendea
Tumwa alimtokea
Kwenye kaburi bilali