PONGEZI MAARUSI

      1 Comment on PONGEZI MAARUSI

Siku imefika, tunafurahia
Tumejumuika, tunasherekea
Raha kwa hakika, imetuenea
Maarusi wetu, tunawapongeza

Leo ‘meungana, kwa njia halali
Muzidi pendana, mapenzi ya kweli
Hadi kwenye janna, muweni wawili
Maarusi wetu, tunawapongeza

Ndoa ni baraka, sunna ilo njema
Na haina shaka, ‘lioa hashima
Twaomba Rabuka, muishi daima
Maarusi wetu, tunawapongeza

Tupo furahani, harusi kucheza
Ni nusu ya dini, muloitimiza
In shaa Allah manani, awape mwangaza
Maarusi wetu, tunawapongeza

Na pia wazazi, pande zote mbili
Twawapa pongezi, kulitenda hili
In shaa Allah mwenyezi,awape sahali
Maarusi wetu, tunawapongeza

Mawadda na rahma, awape manani
Ndoani daima, muwe furahani
Muishi kwa wema, bila tafrani
Maarusi wetu, tunawapongeza

Muite vizuri, mwenza afurahi
Majina mazuri, si ya ikirahi
Izidi sururi, kumuita ruhi
Maarusi wetu, tunawapongeza

Walo wema wana, walosuluhia
Mola subuhana, kuwajaalia
Ya kusikizana, iwe familia
Maarusi wetu, tunawapongeza

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

1 thought on “PONGEZI MAARUSI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *