
Ndoa ni Jambo la kheri, Sunna ya wetu hashima
Na tena ni jambo zuri, twapaswa kuliegema
Tutaipata sururi, kuepuka uhasama
Lakini zisitughuri, harusi zenye gharama
Swali ninalikariri, nijibuni enyi umma
Eti harusi nzuri, ni zenye kubwa gharama?
Kwa watu ujifakhiri, na sifa kukuandama
Ni kwanini zitughuri, harusi zenye gharama?
Vyakula vilo kathiri, kuku pilau na nyama
Twaona ni uhodari, kutoa bila kukoma
Tufahamuni vizuri, israfu sio njema
Jamani zisitughuri, harusi zenye gharama
Veli kutoka qatari, viatu toka Dodoma
Sio mwisho wa habari, harusi wiki nzima
Kisha twaomba qahari, abariki ndoa jama!
Wakati zimetughuri, harusi zenye gharama
Na holi la kifahari, la pesa chungu nzima
Mamilioni si siri, twakopa tena Kwa hima
Hapo twaiwasha nari, au mwadhani twaizima?
Jamani zisitughuri, harusi Zenye gharama
Harusi kiwa swaghiri, twajiona tuko nyuma
Eti haiwi nzuri, pia watu watasema
Hivi humchi qahari, wacha watu kulalama?
Ni majonzi ‘metughuri, harusi zenye gharama
Tuifahamu safari, si siku ni ya daima
Kwa hiyo tutafakari, tusije chanda kuuma
amri zake qahari, tufuate hima hima
‘sikubali zitughuri, harusi zenye gharama
Harusi ndogo tukiri, ndizo zenye usalama
Hasadi na zote shari, na hazitotugandama
Mambo yatakuwa shwari, Kwa uwezo wa karima
Kwa hivyo zisitughuri, harusi zenye gharama