Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Waandishi wetu mbuji, waloandika vitabu
Walivyo navyo vipaji, hakika ni vya ajabu
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Nawavulia kofia, waandishi wetu aali
Vyema ‘metuandikia, vitabu aina mbali
Tena ninavisifia, vitamu kama asali
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Kianza na walibora, asifika duniani
Uandishi wake bora, asoujua ni nani
Kipaji chake chang’ara, mfano mwezi angani
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Mwengine Omari babu, gwiji sio masikhara
Vitamu vyake vitabu, hususan heri subira
Kuvisoma sio tabu, hata milioni mara
Nawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Na Mohamedi saidi, mwandishi wa utengano
Uandishi maridadi, mazuri yake maneno
‘kisoma utaburudi, pia ufungue meno
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Mwengine suleimani, kiu aloiandika
Mwandishi aso kifani, kote kote asifika
Vitabu vyake mwendani, kuvisoma hutochoka
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Na saidi Abdulla, vitabu vyake ni vingi
Mfano ulio aula, ni kisima cha giningi
Wasomaji hala hala, tuvisomeni Kwa wingi
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Hubaki kutabasamu, pia huwa furahani
Kiwaza riwaya tamu, za mwandishi wetu beni
Salamu toka kuzimu, huniacha taabani
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Ninampatia tuzo, mwandishi alo kigogo
Riwaya zenye mafunzo, katuandikia mbogo
Faida ni mzo mzo, kwenye vipuli vya figo
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu
Na rayya timami pia, nadhani twamtambuwa
Kweli ‘metuandikia, hadithi zilo muruwa
Siachi kuzisifia, ni tamu kama haluwa
Ninawavalisha taji, taji lilo la dhahabu