Utaishi na rafiki, umfanye kama ndugu
Uzidishe itifaki, muishi pasi vurugu
Kumbe ndani ana chuki, ana na mengi mathungu
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Utampenda kikweli, na pia umuamini
Ufanye kwa kila hali, ili awe furahani
Kumbe mwenzio katili, ana kinyongo moyoni
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Kiumbe alo hatari, kuliko simba na chui
Usoni huwa mzuri, ila moyoni humjui
Huua kisiri Siri, mche kuliko adui
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Umsafie na Nia, wajua ni mwenzi wako
Mambo yako wamwambia, hata zile siri zako
Kumbe yeye aumia, ayapata maudhiko
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Na wengineo ni panya, wauma wakivuzia
Daima wahanya hanya, maovu kuyafichia
Watamani pata mwanya, mabaya kukufanyia
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Na unapofanikiwa, ni wa kwanza kumwambia
Moyoni mwako wajuwa, kuwa atafurahia
Kumbe usilolijuwa, mwenzio amechukia
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Akiona umefeli, hufurahika moyoni
Akafanya na kejeli, eti anayo huzuni
Abadani hakujali, raha yake uwe chini
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu
Ukipatwa na mikasa, moyo wake humtuwa
Atamani hata fursa, ya kabisa kukuuwa
Avifanya vingi visa, bila ya wewe kujuwa
Ungamuona ni mbuzi, kumbe ndani mbwa mwitu