NANI WA KULAUMIWA?(MALEZI)

      No Comments on NANI WA KULAUMIWA?(MALEZI)

Nimeketi na kuwaza, majibu nikayakosa
Kunyamaza sikuweza, kwa ‘livokithiri visa
Hivyo sauti napaza, nijibuni enyi insa
Wana ‘kikosa mwangaza, nani wa kulaumiwa?

Wana ‘kiwa watukutu, wakafanya yaso ndia
Nyoyo zikajaa kutu, zikawa mbovu tabia
‘kipotoka wana wetu, nani huwa kachangia
Nijibuni enyi watu, nani wa kulaumiwa?

Kulitafuta siathi, jibu langu la murua
Hebu nikae tiathi, niwaze na kuwazua
Nisaidie kathithi, ukweli kuutambua
Mwana ‘kiwa afirithi, nani wa kulaumiwa

Wakiwa walevi wana, hawatamu hawanyamu
Watenda yaso maana, wazazi hawaheshimu
Hawamchi subuhana, kutwa kucha ni stimu
Nimekorogeka sana, nani wa kulaumiwa?

Labda tuseme wazazi, ndio wanaochangia
Mwana akiwa jambazi, mama kati hungilia
Atawahonga walinzi, mwana kumuachilia
Hivi mwadhini malezi, ndiyo yakulaumiwa?

Au mama aso mikazo, hatilii maanani
Haweki msisitizo, elimu hasa ya dini
Baba hanayo likizo, daima yuko kazini
Wazazi waso mikazo, ndio wa kulaumiwa?

Mwana atoka nyumbani, mama hata haulizi
Akirudi ni jioni, aleta vitu vya wizi
Mama huwa furahani, akaanza matumizi
Wazazi hivi mwadhani, ndio wa kulaumiwa?

Pia kunao wazazi, bidii ‘meshikilia
Mazuri yao malezi, elimu pia tabia
Nyumba haina upuzi, ila doa ‘meingia
Naomba ufafanuzi, nani wa kulaumiwa?

Wazazi wanateleza, pasi na wao kujua
Kiukweli wajikaza, kueka mambo murua
Ila kuna walosaza, kuombea wana dua
Siachi kuwauliza, nani wa kulaumiwa?

Pengine niwashitaki, wa watoto maswahibu
Si wazuri marafiki, wanetu huwaharibu
Lakini neno sitaki, wana hawaezi jibu?
Ndugu nipe uhakiki, nani wa kulaumiwa?

Au tuseme walimu, kwani wao ndio nguzo
Tena ni lao jukumu, kuwapa wana mafunzo
Vijana vichwa vigumu,wanaweka mapuuzo
Kweli mwadhani walimu,ndio wa kulaumiwa?

Tuseme ni serikali,ndio wanaochangia
Hakuna sheria kali, za adabu kuwatia
Wana bila ya kujali, maovu wajifanyia
Jibuni wasema kweli, nani wa kulaumiwa?

Kiukweli mada hii, mno mi hunichanganya
Au jibu ni jamii, maovu ilokusanya
Wana nao hawatii, machafu wanayafanya
Ndugu mwadhani jamii, ndiyo ya kulaumiwa?

Nimekuna kichwa changu, hadi mvi ukamea
Sijapata jibu langu, swali limenilemea
‘mechoka akili yangu, kuchizika nachelea
Nijibuni wenzi wangu, nani wa kulaumiwa?

Kadi tama nimefika, japo jibu sijapata
Moyoni ninakereka, na matumbo kunikata
Wanetu kuharibika, ni suala lilo tata
Tumtafute hakika, mtu wa kulaumiwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *