JINSI YA KUTENGEZA PILIPILI MBUZI ZA KUSAGA

Wapo wanaomini kuwa mlo wowote huwa haujakamilika iwapo hakutakuwa na pilipili pembeni. Hawa ndio maashiki wakuu wa pilipili. Pilipili kwao ni kama injini ya gari, yaani mambo katika mlo hayaendi sawa bila pilipili.  Lakini pia wapo baadhi wanaoiona pilipili kama adui shadidi kwao. Iwapo unataka wasile basi wajazie pilipili kwenye chakula na hawatakigusa hata kwa dhihaka. Naam, kila mtu ana mtizamo wake katika ulaji wa pilipili. Hali kadhalika wapo wengine wanaoshindwa kuelewa ni kwa nini watu wajitese Kwa kutia kitu ambacho wanajua fika kitawaletea muasho vinywani mwao. Kwa nini wale pilipili alafu waanze kujipepea vinywa? Lakini wao wenyewe watakwambia kuwa huko kuwashwa ndio raha yake.

Mimi binafsi pilipili ni mwendani wangu kipenzi. Chakula kwangu hakishuki bila pilipili. Hata hivyo, pamoja na mapenzi yangu shadidi ya pilipili, pilipili mbuzi nazivulia kofia. Kuimaliza pilipili mbuzi moja kwangu ni mtihani mkubwa. Kwa hakika muasho wake sijapata kuona. Naam, kama sijakosea utafiti unatuthibitishia kuwa pilipili mbuzi ndizo pilipili zinazowasha kuliko pilipili zote ulimwenguni. Loh! Nadhani hilo linawalete taswira flani ya jinsi pilipili hizi zinavyoweza kumfanya mtu akawa mwendawazimu. Hata hivyo, pilipili hizi zina harufu kuntu ambayo kwamba bila shaka ndiyo inayowapendeza wengi na kuwafanya wazienzi pilipili hizi licha ya muasho wake wa kumchezesha mtu densi.

Anha! Mgala muue na haki yake umpe. Pamoja na pilipili mbuzi kuwa na muasho wa ajabu na wengine kuziona kama sumu hasa, vile vile zina faida ainati katika mwili wa binadamu. Kwanza kabisa kiungo kinachopatikana katika pilipili kiitwacho ‘capsaicin’ kinapunguza kolestro mwilini na shinikizo la damu. Aidha zinasaidia kupunguza uzito wa mwili, inastaajabisha ebo Lakini ndio ukweli halisi. Vile vile pilipili mbuzi zinasaidia kuzuia saratani. Mchanganyiko wa vitamini A, C na ‘capsaicin’ unazuia ukuaji wa seli za saratani.

Hivi majuzi kumeletwa pilipili mbuzi nyumbani na nikaonelea nizisage pamoja na malimau. Ungana nami tujifunze jinsi ya kutengeza pilipili hii.

MAHITAJI

  • Pilipili mbuzi
  • Maji ya malimau/ ndimu 5 yaliochujwa kokwa zote
  • Vitunguu maji 2
  • Kitunguu thomu konde 6
  • Siki kiasi
  • Chumvi

MATAYARISHO

  • Katakata vitunguu maji na vitunguu thomu ili iwe rahisi katika kusaga

  • Weka kila kitu kwenye blender na usage vizuri.
  • Baada ya hapo pilipili ipo tayari.
  • Unaweza ukala pilipili hii Kwa viazi karai, bajia au chakula kingine chochote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *