JINSI YA KUPIKA CHAPATI LAINI SANA KWA KUTUMIA UNGA WA MAZIWA

Chapati ni chakula maarufu sana kote ulimwenguni na ni chakula kikuu cha India, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal. Licha ya chakula hiki kupendwa na wengi, ndicho chakula kinachowapa wengi changamoto. “Mbona chapati zangu huwa ngumu Sana?” ,”Chapati zangu zinakuwa kavu kama papuri” ,  “Mimi napata shida sana katika kusukuma chapati zangu.” “Aaah zangu hazifanyi kurasa.” Haya ni miongoni mwa malalamishi  ya wengi ambao kwamba wana hamu ya kupika chapati tamu. Naam, chakula chochote bila shaka kinapendeza kinapopikwa kwa njia inayostahiki na kuzingatia vigezo muhimu.

Binafsi chapati ni miongoni mwa vyakula ninavyovifurahikia sana kuvipika na kuvila vile vile. Nakumbuka nilipokuwa mdogo sana na ndio mwanzo naanza kujifunza kupika nilikuwa nikitaka kupika mpaka niulize kiasi cha viungo takriban vyote, mathalan chapati nitauliza, “hii samli imetosha? Chumvi kiasi hiki ni Sawa? Unga umekandika?” Jambo hilo lilikuwa likinikera mno na kutamani ifikie siku ambayo nitaweza kupika mimi mwenyewe kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kwa juhudi mzo mzo niliweza kulifanikisha hilo.

Leo nitawafunza njia rahisi sana ya kupika chapati zitakazokufanya usile tena kwa mama ntilie au kama wewe ni mfanyibiashara wa chapati basi wateja wamiminike kununua chapati zako. Nilijaribu mbinu nyingi sana za kupika chapati lakini hazikunipendeza. Hatimaye nilifunzwa mbinu hii na mama yangu na nikayapenda sana matokeo yake.

MAHITAJI

 • Unga vikombe 2&1/2
 • Samli vijiko 2 vya mezani iliyoekwa motoni
 • Unga wa maziwa vijiko 2 vya mezani(inasaidia kulainisha chapati zaidi)
 • Chumvi kiasi
 • Maji kiasi

MATAYARISHO

 • Weka chumvi na unga wa maziwa kwenye unga uchanganye vizuri
 • Weka samli uchanganye mpaka mavumbo yote yaishe(unaweza ukauchuja unga ili kuhakikisha kuwa mavumbo yote yameisha)
 • Weka maji kidogo kidogo ukiendelea kukanda unga wako mpaka ushikane (hakikisha unga wako hauwi mgumu)

 

 • Ueke unga wako katika bakuli ulilolipaka mafuta uufunike na uuache Kwa takriban nusu saa au zaidi. Ukiuacha Kwa muda mrefu zaidi ndiyo bora zaidi kwasababu utalainika zaidi.

 

 • Gawanya unga wako madonge mawili tayari kufanya tabaki. Kufanya tabaki kunasaidia chapati kufanya kurasa.
 • Sukuma donge moja na upake samli au mafuta juu

 • Kunja na ukate vipande vya kiasi
 • Chukua kipande kimoja kimoja ukunje kama dawa ya mbu(coil)na uzifunike uziache Kwa nusu saa au zaidi

 

 • Sukuma chapati moja moja kiuduara. Kama unga wako ulikandika vizuri basi hautakupatia shida kabisa katika kusukuma

 

 • Bandika chuma motoni(frying pan) na kikishashika moto weka chapati ulioisukuma
 • Ikishapata rangi upande mmoja igeuze upande wa pili
 • Paka samli uipike upande mmoja huku ukiemeza emeza chini mpaka ikolee rangi vizuri
 • Geuza upande wa pili ufanye vivyo hivyo
 • Endelea vivyo hivyo Kwa chapati zote
 • Chapati zipo tayari
 • Andaa Kwa chai ya mkandaa, mchuzi wa viazi au Maharagwe.

KWA MAELEZO ZAIDI UTANIPATA

 • Instagram@farwats_kitchen
 • Facebook@farwat’s kitchen

You tube@farwat’s kitchen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *