JINSI YA KUPIKA MATOKE

      No Comments on JINSI YA KUPIKA MATOKE

Matoke, matooke au ibitoke ni chakula Chenye asili ya kiganda. Hata hivyo, wanavyopika waganda na tunavyopika sisi wakenya ni tofauti. Waganda aghlabu huyapika Kwa mvuke tu ilhali  wakenya mpaka tuyapambe kwa viungo tofauti tofauti. Aidha zipo njia nyingi sana za kuzipika ndizi hizi mbichi. Unaweza ukazikaanga, kuzichemsha na kuziponda, ukapika vibanzi kama wafanyavyo watu wa nchi ya Kerala au ukaziunga kutumia mahitaji mengine kama wafanyavyo wakenya wengi. Yote tisa, kumi matooke ni chakula maarufu sana Kenya na kinachoenziwa na wengi. Kwanza kabisa, ni rahisi sana kukipika, ni kitamu ajabu na pia kinapatikana Kwa bei ambayo kwamba wengi wanaweza kuimudu. Binafsi kama kuna vyakula naweza kuvifurahia hata vikikaa kwenye jokofu kwa wiki nzima basi miongoni mwavyo ni matoke😂. Matoke ni chakula ambacho kwamba hakikinaishi wala hakichoshi abadaan kataan.

Pamoja na ladha yake muruwa, matoke vile vile yana faida aina aina za kiafya. Kwanza yanasaidia kupunguza uzito kwa kudhibiti upataji wa kalori. Hivyo basi, kama upo katika harakati za kupunguza uzito usisahau kuyaweka matoke katika ratiba yako. Vile vile, ni chanzo cha vitamini na potasiamu ambayo kwamba inasaidia kupunguza shinikizo la damu. Aidha, ni chanzo cha faiba ambayo ni muhimu Kwa wenye tatizo la mmeng’enyo na kuvimbiwa. Wanga unaopatikana ndani ya matoke husaidia kuboresha sukari ya damu. Pia matoke husaidia kuboresha uwezo wa mwili kupata virutubisho hasa hasa kalsiamu.

Bila kupoteza muda, twende moja Kwa moja katika maandalizi ya chakula hiki

VINAVYOHITAJIKA

 • Matoke(ndizi mbichi) 12 kubwa
 • Viazi kilo 1 & 1/2
 • Nyama  1/2 kilo
 • Tomato 4 zilizokatwa katwa au kusagwa
 • Karoti 1 kubwa iliyokatwa katwa
 • Dania 1
 • Pilipili boga/hoho 1 lililo katwa katwa
 • Tomato paste/tomato ya mkebe(sio lazima)
 • Kitunguu thomu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
 • Pilipili manga kijiko 1 cha mezani
 • Currypowder vijiko 2 vya mezani
 • Chumvi kiasi
 • Mafuta ya kupikia/ uto vijiko 2 vya mezani

MATAYARISHO

Bandika sufuria motoni ueke mafuta na yakishika moto weka Kitunguu maji. Kitunguu kikikaribia kuwa hudhurungi(golden brown), weka pilipili manga, currypowder na Kitunguu thomu upike Kwa sekunde kadhaa. Kisha weka karoti, pilipili boga na dania pia uzipike Kwa sekunde kadhaa

Weka tomato pamoja na chumvi (na tomato ya mkebe ukipenda kisha ufunike upike Kwa takriban dakika 3_5 au mpaka tomato ziive na zikauke maji

Weka nyama na supu yake pamoja na matoke na viazi. Kama nyama yako imelainika sana unaweza ukaiacha uitie matoke na viazi vitakapoiva. Pia, weka matoke na viazi kwa wakati mmoja kwasababu vinachukua muda takriban sawa kuiva. Kisha weka maji kiasi ambacho kitasaidia matoke kuiva.

Funika matoke yako uyaache Kwa takriban dakika 15_25(mpaka viazi na matoke vilainike)

Matoke yapo tayari. Unaweza ukayaacha na maji mingi kiasi kama unataka yawe na rojo jingi au ukayaacha yawe makavu. Pia unaweza ukaweka royco na kuyaacha yatokote kwa dakika mbili. Andaa mezani kwa limau au achari ya ndimu na juisi ya pesheni.

KWA MWPISHI ZAIDI UTANIPATA

 • Instagram@farwats_kitchen
 • Facebook@farwat’s kitchen
 • You tube@farwat’s kitchen

❤❤❤

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *