
RUIYA
Mume wangu sikiliza, nisemayo usikie
Nakupa yenye mwangaza, yatakuja yakufae
Wewe ni mwenye uweza, naomba ufikirie
Rafiki yangu Aziza, ningependa umuoe
Sana ninapendekeza, hili ulizingatie
Ukae ukiliwaza, moyoni likuingie
Pia nakusisitiza, haraka ujiandae
Rafiki yangu Aziza, ningependa umuoe
Najua unayaweza, nakuelewa mwenyewe
Na Mola Takuongoza, wala shaka usitie
Nami nitawaeleza, wazaziwe waelewe
Rafiki yangu Aziza, ningependa umuoe
Kwa uchache namaliza, mengi nisiyaongee
Najua tanisikiza, na mema ujifanyie
Kheri ukitekeleza, Mola yuko radhi nawe
Rafiki yangu Aziza, ningependa umuoe
FARWAT
Ewe dada nisikiza, na tena uwe makini
Yasije yakakuliza, ukaumia moyoni
Si rahisi uke wenza, hilo tia fahamuni
Akiolewa Aziza, utangia majutoni
RUIYA
Huenda yakaniliza, nikangia majutoni
Lakini Mola muweza, ndiye ninamuamini
Tanipa nami uweza, wa kulibeba moyoni
Akiolewa Aziza, nitakuwa furahani
FARWAT
Ni sheria ya Muweza, sikatai abadani
Ila ukimuhimiza, mume tapanda kichwani
Ye hataki kuongeza, wamlazimishiani?
‘Kija nyumbani Aziza, utaumia mwendani
RUIYA
Japo ningayakataza, kukataa asilani
Akitaka kuongeza, hatoyajali maoni
Ngafikia kujiliza, na kuondoka nyumbani
Na amuoe Aziza, roho yangu i makini
FARWAT
Naona umeikaza, kanga yako kiunoni
Katu hutonisikiza, abadani kataani
Kama kweli ‘tayaweza, basi ngia uwanjani
Na aolewe Aziza, sisi tuje harusini🤣🤣🤣
RUIYA
Ngependa kukuuliza, kwani tatizo ni nini?
Wa pili akiongeza, mimi nitapunguani?
Kule kipeleka pweza, huku taleta maini
Na amuoe Aziza, rafiki yangu mwendani
FARWAT
Ewe dada nisikiza, waume wa karne hini
Ikiwa tacheza cheza, watakufika kooni
Uadilifu ‘mesaza, wala hawauthamini
‘tapendwa mno Aziza, wewe upigwe na chini
RUIYA
Haliwezi nitatiza, kubabaisha moyoni
Mwenzangu ninakujuza, sana ninajiamini
Hapa hakuna kucheza, ni full time kazini
Muache aje Aziza, mimi ndio namba wani
FARWAT
‘memkubali Aziza, rafiki yako mwendani
Mimi nimeshakujuza, nikakupa na ilani
Kibwebwe basi jikaza, ubakie namba wani
Hata akija Aziza, usiumie moyoni
RUIYA
Sasa umezungumza, maneno yalo makini
Meuona muangaza, mekungia fahamuni
Harusi ninakujuza, itakuwa karibuni
Ataolewa Aziza, tukae sote nyumbani
Mash Allah umeweza dadangu Mungu akuzidishie insha’Allah
Shukran
Aaamiiin