JINSI YA KUPIKA MAYUNGU/MATANGO YA NAZI

Hivi ushawahi tafakari ni nani aliyekaa akawaza na kuwazua mpaka akaleta fikra ya kuchanganya viungo tofauti tofauti na hatimaye kuunda chakula kitamu sana? Ni nani aliyewaza kuwa ukichanganya mayungu na nazi na sukari basi kutazalika chakula Chenye ladha ya kumuamsha alalaye? Yeyote yule awaye, tunamvulia kofia.

Kiukweli mimi si mlaji sana wa vyakula vya sukari ila nimetokea kuwa ashiki shadidi wa mayungu ya sukari na nazi.. Nakumbuka enzi zile mayungu yalipokuwa yakipikwa aghlabu wakati wa Ramadhani mpaka nikajenga fikra kuwa mayungu ni ya
Ramadhani pekee. Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa hata mala mthana mayungu hupikika, ikawa natamani niyapike takriban kila siku. Siku mama yangu akileta mayungu nyumbani, basi huwa na furaha ghaya kushinda tasa aliyejifungua pacha. Siku hiyo nitakuwa mwenye kutabasamu mchana kutwa. Naam, bila shaka chakula chochote kikipwa kwa njia aula basi mtu yeyote huenda akajikuta katika mapenzi mubashara na chakula hiko. Hivyo basi, ungana nami tujifunze kupika mayungu kwa njia rahisi na ambayo kwamba itakufanya ukipende chakula hiki hata kama ulikuwa hukipendi hapo awali.

Naam, pamoja na chakula hiki kuwa na ladha ya kipekee, vile vile kina faida sufufu katika mwili. Kwanza kabisa kina virutubisho ambavyo kwamba vinahitajika sana katika mwili wa binadamu. Vile vile, kina vitamini na madini aina aina na kalori inapatikana Kwa uchache mno ndani yake. Aidha, potasiamu inayopatikana ndani ya mayungu ina athari chanya katika shinikizo la damu. Utafiti pia unatuthibitishia kuwa kuwa mayungu yanapunguza fetma na kuzuia kisukari pamoja na maradhi ya moyo. Hizo ni faida chache miongoni mwa nyingi zinazopatikana katika mayungu.

MAHITAJI
▪ Mayungu/ matango  yaliokatwa maganda, kukatwa vipande vipande na kuoshwa vizuri
▪ Sukari kiasi
▪tui jepesi vikombe 2
▪tui zito kikombe 1
▪Iliki
▪ vanilla (sio lazima)

MATAYARISHO

 • Weka sukari, iliki na tui jepesi kwenye mayungu. Naam, ni rahisi mno, waonaje?

 • Yaache yatokote mpaka maji yakauke na mayungu yalainike. Usiweke tui jepesi jingi mpaka mayungu yakalainika kupita kiasi. Mayungu hayachukui muda mwingi kulaininika, hivyo basi maji au mathusha kidogo yanatosha kuyaivisha.

 • Weka tui zito na vanilla na uache ichemke Kwa dakika 1. Hii ndiyo hatua ya mwisho na muhimu sana. Tui zito utakalotia wakati huu ndilo linaloleta ladha bulbul ya chakula hiki.

 • Mayungu yapo tayari
 • Andaa mezani Kwa chai ya mkandaa

KWA MAPISHI ZAIDI UTANIPATA

 • Instagram@farwats_kitchen
 • Facebook@farwat’s kitchen
 • You tube@farwat’s kitchen

❤❤❤

 

 

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

3 thoughts on “JINSI YA KUPIKA MAYUNGU/MATANGO YA NAZI

 1. Rehema

  MashaALLAH chakula kizuri sana ukhty hata mie nlikua ckifaham.

  ALLAH akupe Afya na umri mref uzidi kutufunza inshaALLAH

  Naomba pia unitumie na vyakula wavipendavyo watu wa pwani(kilwa) maana mume wangu mtu wa huko.
  Shukran ukhty.

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *