TABASAMU

      2 Comments on TABASAMU

Naanza yangu nudhuma, hali nikitabasamu
Natumai mu wazima, ndugu ninawasalimu
Basi simameni wima, kusikiza ya muhimu
Awe mwendani daima, anoitwa tabasamu

Usimbanduke katu, awe usoni dawamu
Hata wakupige watu, na pia kukushutumu
Wakurushie viatu, na mno kukudhulumu
Kumuacha ‘sisubutu, anoitwa tabasamu

Ni kweli kuna wakati, maisha huwa magumu
Yakakupiga vibati, ukaishiwa na hamu
Miezi hata sanati, ni shida zamu kwa zamu
Hata hivyo jizatiti, ‘sishopoke tabasamu

Lolote linokufika, ni mtihani fahamu
Ni Jambo lisilo shaka, imeandika kalamu
Ni mipango muafaka, ameyapanga rahimu
Siwe utahuzunika, ewe ndugu tabasamu

Madhila yanapokuja, jua hayawezi dumu
Baada dhiki faraja, chungu itakuwa tamu
Kuwa na imani mja, kwa qudura ya karimu
Mpige kubwa pambaja, swahibayo tabasamu

Ndugu usiwaze sana, ‘kikusonga majukumu
Fahamu ewe kijana, mawazo mengi ni sumu
Sijione huna mana, na mno kujihukumu
Elekea Kwa rabana, adumishe tabasamu

Maisha ‘kiwa subili, hayatamu hayanyamu
Sijione u dhalili, mambo yako kutotimu
Aso lile ana hili, hilo swahibu fahamu
Shukuru kwa kila hali, na pia utabasamu

Nimefika kikomoni, mwisho wa yangu nudhumu
Kwaherini ikhiwani, nawaaga kwa nidhamu
Jina langu ndilo gani? Ni farwatha qaumu
Na ninawakumbusheni, tuzidi kutabasamu

2 thoughts on “TABASAMU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *