JINSI YA KUPIKA KATLESI ZA KUKU

Kama wanavyosema, mama ndiye mwalimu wa kwanza. Kwangu mimi, mama yangu amekuwa mwalimu muhimu katika maisha yangu. Amenifunza mengi yenye manufaa na miongoni mwayo ni mambo ya jikoni. Nimejifunza mapishi aina aina pamoja na mambo mengi muhimu ya  kuzingatia jikoni na bado naendelea kujifunza kupitia kwake. Aghlabu ninapokuwa naye jikoni, ima nitajifunza mapishi mapya au mbinu mpya katika mapishi. Naam, ninapopata ujuzi flani kutoka kwake basi nami hupenda kuusambaza kwenu pia mashabiki zangu ili tujifunze kwa pamoja. Leo hii nitawaonyesha mapishi ya katlesi za kuku ambayo kwamba sikuwahi kuyafkiria hapo awali. Katlesi nilizozizoea sana ni za kima ila hivi majuzi mama yangu amenionyesha ujuzi mpya wa katlesi za kuku nami nikaona haitakuwa vyema lau sitowapeni nanyi ujuzi huu. Ungana nami tujifunze kwa pamoja!

MAHITAJI

 • Viazi kilo 2 vilivyochemshwa na chumvi na kupondwa
 • Kuku(Yule mzima utamgawanya nusu yake) umtoe steki yote kisha ichemshe na chumvi na thomu mpaka ilainike na akauke maji
 • Vitunguu maji 2 vikubwa vilivyokatwa katwa vidogo vidogo
 • Pilipili boga/hoho/bofu 1 lililokatwa katwa vidogo vidogo
 • Dania moja iliyokatwa katwa
 • Carrot 1 kubwa iliyochambuliwa maganda na kugretiwa(Kwa urefu)
 • Pilipili manga kijiko 1 kodogo
 • Currypowder kijiko 1 kidogo
 • Dania ya unga kijiko 1 kidogo
 • Limau/ndimu 2
 • Yai 1
 • Mafuta uto(ya kupikia) ya kukaangia katlesi

MATAYARISHO

 • Kamulia limau kwenye viazi ulivyoviponda, changanya vizuri kisha weka pembeni.
 • Umtoanishe kuku uliyemchemsha mpaka awe vipande vidogo vidogo
 • Weka viungo vyote ndani ya kuku kisha umbandike tena motoni Kwa dakika 2
 • Chukua viazi kiasi ufanye round ndogo, kisha toboa shimo katikati uweke nyama ya kuku na ufunike vizuri. Rejelea hatua hii Kwa viazi vyote
 • Piga yai moja utie chumvi kidogo Sana kisha lichanganye vizuri
 • Bandika mafuta motoni mpaka yashike moto
 • Chovya katlesi kwenye yai kisha zichome
 • Zikishika rangi upande mmoja, zigeuze upande wa pili
 • Zitoe kwenye mafuta na zipo tayari
 • Andaa mezani Kwa juisi ya passion

MAELEZO MUHIMU

 • Hakikisha mafuta kwenye karai ni mengi kiasi cha kufunika katlesi. Mafuta yakiwa kidogo na sehemu ya katlesi ikiwa inaonekana juu huenda zikapasuka
 • Viponde viazi vikiwa moto kwasababu vinapondeka Kwa urahisi vikiwa moto
 • Wakati wa kufunga katlesi, hakikisha unazifunga vizuri ili sehemu nyingine isiwe nyembamba kiasi cha nyama kuonekana. Hii huenda ikasababisha katlesi kupasuka
 • Ukienda kununua viazi sokoni, nunua viazi vya katlesi au vya unga kwasababu kuna baadhi ya viazi vinanyata na si vizuri kufanyia katlesi
 • Viazi vikishaiva hakikisha unamwaga maji yote kabla ya kuviponda ili visikupe shida wakati wa kufunga katlesi.

KWA MAPISHI ZAIDI UTANIPATA

 • Instagram@farwats_kitchen
 • Facebook@farwat’s kitchen
 • You tube@farwat’s kitchen

❤❤❤

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *