VISIWA VYA KOMORO

      No Comments on VISIWA VYA KOMORO

Unajua nini kuhusu visiwa vya Comoros? Au pengine ushawahi sikia jina Comoros na ukashangaa ni nchi gani hiyo na inapatikana sehemu gani ya dunia? Unazijua mila zao japo mbili tatu? Ushawahi tamani kutembelea visiwa hivyo? Wapo walio na kiu kuu ya kufahamu mengi kuhusu Comoros na kama wewe ni mmoja wao basi makinika nami tuikate kiu hiyo. Vile vile, wapo wanaotamani kwenda kuifurahikia fungate yao Comoros. Mmh! Hiyo fikra ishawahi kukupitikia? Kama bado, soma makala haya na huenda ukabadili nia kama ulikuwa na nia tofauti.

Comoros ni kisiwa katika bahari hindi kinachopatikana mashariki mwa Mozambique na kaskazini_magharibi mwa Madagascar. Jina Comoros limetokana na neno la kiarabu ‘qumr’ linalomaanisha mbalamwezi. Kisiwa hiki kimegawanyika zaidi katika visiwa vitatu ambavyo kwamba ni Ngazidja, Mwali na Nzwani. Ngazidja ndicho kisiwa kikubwa zaidi kuliko vyote ndani ya Comoros. Mji mkuu wa Comoros ni Moroni na unapatikana katika kisiwa cha Ngazidja. Lugha zinazozungumzwa katika nchi hii ni kiarabu, kifaransa na Shikomoro ambayo kwamba inafanana lakini haihusiani na Kiswahili. Vile vile, ndiyo lugha inayozungumzwa zaidi kuliko lugha nilizozitaja hapo juu zinazotumika kisiwani humo. Kila kisiwa kina namna yake ya kuzungumza lugha ya Shikomoro na maneno yake mengi ni yenye asili ya kiarabu na kifaransa. Hata hivyo, shuleni wanafunzi hufunzwa kwa lugha ya kifaransa.

Dini iliyotawala katika visiwa vya Comoros ni uislamu na hususan uislamu wa Sunni. Wengi wao hujifunza Qur’an pamoja na herufi za kiarabu licha ya kuwa elimu ya shuleni hufunzwa kwa kifaransa. Hata hivyo, wacomoro wameathiriwa mno na tamaduni za Kiarabu, kifaransa na kimagharibi kwa ujumla.

Muacha mila ni mtumwa ebo! Na wacomoro hawakukubali abadani kuipuuzilia mbali methali hiyo. Comoros ni kisiwa kilicho na utajiri wa mila na tamaduni aina aina. Kwanza kabisa ni vyakula vyao ambavyo kwamba wanavipika kwa ustadi wao wenyewe. Tukianza na wali ambao kwamba aghlabu huliwa kwa nyama ya mbuzi na maziwa mala hasa katika sherehe zao. Chakula kingine kilicho maarufu mno kisiwani humo ni ndizi hususan ndizi za mkono wa tembo na samaki. Hapo nimewapatia maarifa flani hivi! Iwapo mutapata wageni wacomoro basi waandalieni vyakula vya aina hii na itakuwa kama mulowaangulia mwezi😅

Tamaduni nyingine ambayo kwamba wakomoro wamekataa kata kata kuibanduka ni sherehe zao za kukata na shoka. Ikiwemo sherehe flani wanayoiita ada ambayo kwamba inafanyika kwa wanandoa wanaotaka kusherehekea tena harusi yao. Pia kuna sherehe za harusi wanazoziita ndoola nkuu na arusi. Katika harusi zao aghlabu huhusishwa dhahabu za bei ghali zinazonunuliwa kutoka Saudi Arabia anazopewa bibi harusi. Haya hala hala kina binti tuoleweni Comoros tujishindie dhahabu hizi.😂

Mila nyingine ambayo kwamba ni maarufu mno kwa wakomoro ni upakaji wa liwa Kwa wanawake. Liwa ni mti flani unaokaa kama mbao hivi unaosuguliwa chini kwa maji kidogo, hatimaye hufanana kama manjano. Aghlabu hupakwa usoni na husaidia kungarisha uso. Wanawake wa kikomoro hupenda sana kuipaka na kutembea nayo njiani au hata wakiwa katika sherehe zao. Hivyo basi, utakapopishana nao wakiwa wamepaka liwa usishtuke na kutoka mbio. Aidha, mavazi yao yanadhihirisha utajiri katika mila zao. Wanawake huvaa shiromeni ambayo kwamba ni nguo ndefu iliyo na rangi za kupendeza pamoja na sketi. Wanaume nao huvaa shati ndefu nyeupe na koffia inayothaminika sana miongoni mwa watu wa komoro

Kabla sijaweka kalamu chini ningependa kugusia mimea inayopatikana kwa wingi katika visiwa vya Comoros. Nayo ni vanilla, karafuu na nazi. Hivyo basi, ukiwa na mgeni kutoka Comoros anayetaka kuja kukutembelea mwambie akuletee vitu hivi na akisema havipatikani huko basi huyo itakuwa amekupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Naam! Hayo ndiyo machache miongoni mwa mengi yanayopatikana katika visiwa vya Comoros.Wenye kunena hunena, heri shi kuliko mash. Hata hivyo, natumai kwa waliokuwa na kiu ya kutaka kuvifahamu visiwa vya Comoros basi kiu hiyo mumeshaikata.

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *