MWANAMKE ASO BADALI_MAMA

      2 Comments on MWANAMKE ASO BADALI_MAMA

Sura umeikunja! Meno umeyakaza! Unabamiza milango na kurusha rusha vitu huku na kule! Mori umekupanda tayari kummeza mzima mzima yeyote atakayepita mbele yako. Kisa na sababu? Mama yako amekuita. Pengine amekuita ulipokuwa ukiangalia filamu yako unayoienzi au ulikuwa katika usingizi mwanana. Vyovyote iwavyo, unapandwa na ghadhabu unapoisikia sauti ya mwanamke adhwimu duniani? Sauti ambayo kwamba wengi wanatamani kuisikia japo Kwa sekunde kadhaa lakini haiwezekani kwasababu mama zao walikwishatangulia mbele za haki? Unaibeza almasi uliyonayo mikononi na kuiona kama takataka? Unathubutu kuifunga njia yako mwenyewe ya kuelekea peponi. Njia ambayo kwamba kwa wengi ilikwishafungwa na Allah kwa kuzichukua roho za mama zao na wanaitamani fursa hiyo lakini wapi! Leo umebahatika kuwa na mama pembeni mwako nawe unamdharau na kutouthamini uwepo na thamani yake? Tanabahika!

Abu Huraira ameripoti kuwa kuna mtu amesema:

Ewe mtume wa Allah, nani miongoni mwa watu anayestahiki kutendewa wema nami? Akasema: mamako, tena mamako, tena mamako, alafu babako, alafu jamaa wako wa karibu kulingana na mpangilio huo (wa ukaribu).
حَدَّثَنَا أَبُو كُرَيْبٍ، مُحَمَّدُ بْنُ الْعَلاَءِ الْهَمْدَانِيُّ حَدَّثَنَا ابْنُ فُضَيْلٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ عُمَارَةَ، بْنِ الْقَعْقَاعِ عَنْ أَبِي زُرْعَةَ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، قَالَ قَالَ رَجُلٌ يَا رَسُولَ اللَّهِ مَنْ أَحَقُّ بِحُسْنِ الصُّحْبَةِ قَالَ ‏ “‏ أُمُّكَ ثُمَّ أُمُّكَ ثُمَّ أُمُّكَ ثُمَّ أَبُوكَ
ثُمَّ أَدْنَاكَ أَدْنَاكَ ‏”‏ ‏.‏
Hii hadithi inaonyesha daraja alizopewa mama na uzito wa kuwatukuza na kuwatendea wema mama zetu. Inasikitisha sana kuwa hata baada ya kudhihirishiwa utukufu na daraja ya mama bado tunapata ujasiri wa kuwatendea mama zetu maovu yasioandikika wala kutamkika. Tumepewa funguo za kujifungulia pepo zetu lakini tunaamua kuzizika funguo hizo katika mashimo yenye vina virefu. Tunaambiwa katika hadithi nyingine…

Amepokea hadithi hii At-Tirmidhiy na akaisahihisha kutoka kwa Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mzazi ni mlango wa katikati ya milango ya pepo, ukitaka upoteze mlango huo au uhifadhi)).

Tunawakebehi mama zetu kisha tunajiuliza ni Kwa nini matatizo ya kilimwengu hayeshi kutuandama. Shuleni nako licha ya kubukua usiku na mchana hatufaulu. Tunatafuta kazi laili wa nahari hatupati. Maradhi ya kila aina yametuandama na kukataa kata kata kutubanduka. Al hasili matatizo moja kwa mbili. Wengi wanakimbilia kusema kuwa wamerogwa, eti mikosi inawaandama. SubhanAllah! Tuzindukeni , tujichunguzeni na kujiangalia vizuri. Je tunazo radhi za mama zetu? Je mama zetu wana furaha na sisi? Tuwahini kabla hatujachelewa kuwaomba radhi mama zetu na kuwatendea wema ili wajivunie na kutuonea fahari badala ya kutuona nuksi katika maisha yao.

Na katika sahihi At-Tirmidhiyyi, kutoka kwa Abdillah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Radhi za Mola zinatokana na radhi za mzazi, na chuki zake zinatokana na chuki za mzazi)

Unapotaka radhi za Allah basi mtendee wema mzazi wako. Hivi unataka radhi za Allah na mzazi wako amechoshwa na vitimbi vyako? Unaamka usiku kuomba maghfira, kumlilia mola wako. Unaswali faradhi na sunna lakini mama yako hayupo radhi na wewe. Vipi utazipata rehma za Allah wakati unamnyanyasa, kumtukana na kumuumiza mama yako kila kuchapo. Mama yako analia kila siku kwasababu yako wewe. Mama yako hana raha ya maisha na chanzo ni wewe. Unamuudhi mwanamke ambaye kwamba ndiyo njia yako wewe ya kuzipata radhi za Allah na unatarajia msamaha kutoka kwake Al_ghaffar? Tuzindukeni ndugu zangu.

Mwenyezi-Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema katika Qur-aan Suratul Al-Israai aya ya 23 kwamba:
{{Amehukumu mola wako kuwa asiabudiwe (yeyote) isipokuwa Yeye (tu) na wazazi watendewe wema, kama mmoja wao amefikia uzee (naye yuko) pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata aah! Wala usiwakemee, na useme nao kwa msemo wa heshima}}

“Aaah maa! Mi nnaingia sasa hivi kutoka skuli hata sijapumzika wanituma!”
“Aaaah mimi nnachoka. Si rimoti iko hapo karibu.” Wangapi tunayatamka maneno haya na hata kishipa hakitupigi? Tunayatamka na kuona kama kitu cha kawaida tu. Mama yako alipitia shida chungu nzima wakati upo tumboni, wakati wa kuzaa na kukulea. Licha ya yote hayo, hakukata tamaa wala hakukuchukia bali alikulea kwa mapenzi na kukukinda usidhurike hata ukucha. Leo hii anakutuma kazi nyepesi nyepesi unatamani kuhama nyumba? Unamrushia maneno makali na kuzungumza naye kwa sauti ya juu kana kwamba unaongea na adui. Tunatakiwa tuwe wanyenyekevu na tuzungumze kwa sauti ya chini na mama zetu. Tuwaambie maneno mazuri na kuwaombea dua. Tuwaombe msamaha pindi tunapohisi tumewakosea. Tuwabusu na kuwatamkia kuwa tunawapenda kila siku. Tusisubiri hadi viti vyao vikawa vyeupe ndipo tukaanza kujuta na kuuma zanda.

2 thoughts on “MWANAMKE ASO BADALI_MAMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *