JINSI YA KUPIKA SAMAKI WA KUKAANGA

Mmh samaki! Samaki ni kitoweo kinachodondosha wengi mate. Wapo wengi wasiokula nyama au kuku ima Kwa kutopenda kwao au kwa maradhi flani ila  tukija kwenye samaki, binafsi sijasikia kama kuna mtu asiyekula samaki.

Nakumbuka miaka kadhaa nyuma nilipokuwa bado shule ya msingi, nilikuwa nikiipenda sana siku ya ijumaa na sababu kuu ilikuwa samaki. Naam!  Kila ijumaa kwetu kulikuwa kukipikwa sima, maharagwe na samaki. Najua ni kinaya kwasababu imezoeleka kuwa ijumaa ni siku ya kupikwa pilau au biriani hasa katika kanda ya pwani lakini kwetu zama hizo ilikuwa tofauti. Wengi katika familia walikuwa wakiufurahikia mno msosi wa ugali, maharagwe na samaki pembeni. Mie nina hakika wengi walikuwa wakikipenda chakula hicho kwasababu ya kuwepo samaki ndani yake, binafsi nikiwa miongoni mwao. Yote tisa, kumi tuanze matayarisho ya samaki wa kukaanga Kwa njia muruwa! Kumbuka! Raha ya samaki ni akolee viungo.

MAHITAJI

 • Samaki 1 mkubwa aina yeyote unayopenda
 • Kitunguu thomu vijiko 2 vya Kula
 • Pilipili manga kijiko 1 cha kula
 • Fish masala kijiko 1 cha Kula
 • Limau/ndimu moja
 • Chumvi kiasi
 • Mafuta ya kukaangia samaki

MATAYARISHO

 • Msafishe vizuri samaki wako, mpige mitai yaani mkate mistari kama 4 hivi pande zote mbili ili viungo viingie vizuri  kisha mgawanye vipande 3 au vipande vyovyote upendavyo
 • Changanya viungo vyote ndani ya kibakuli
 • Mpake viungo samaki wako vizuri na uhakikishe vinaingia kila sehemu
 • Weka mafuta kwenye karai au chuma cha chapati kilicho kizito kisha weka motoni( usitie mafuta mengi ili kutahadhari mafuta hayachafuki mengi)
 • Mafuta yakishika moto, weka samaki uwakaange (Moto uwe wa kiasi ili waive vizuri ndani)
 • Wakishawiva upande mmoja, wageuze upande wa pili pia wawive na kushika rangi nzuri ya hudhurungi
 • Watoe kwenye mafuta uwaweke kwenye chombo cha kuchujia mafuta au hata kwenye sahani uliyoitandika tissue paper
 • Samaki wako tauata. Andaa mezani Kwa sima na kachumbari.

KWA MAPISHI ZAIDI UTANIPATA

 • Instagram@farwats_kitchen
 • Facebook@farwat’s kitchen
 • You tube@farwat’s kitchen

❤❤❤

6 thoughts on “JINSI YA KUPIKA SAMAKI WA KUKAANGA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *