
Siku alopanga Mungu, mie nije duniani
Ulimshika uthungu, hali yake taabani
‘kavumilia mamangu, hadi ‘katoka tumboni
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Tarehe kumi na tatu, na mwezi ni Aprili
‘kazawa mwana wa tatu, kwa uwezo wa jalali
Usiwe mwaka wa kutu, ya rabbi nipe sahali
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Nikafika duniani, tumboni nikapaatha
Na jina wakanipeni, nikaitwa farwatha
Mama ‘kawa furahani, kama alopata patha
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Imani iongezeke, na subira kadhalika
Maovu niyaepuke, nayo mema kuyashika
Vishawishi nivivuke, yasinifike mashaka
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Nayo bidii nitie, katu nisilaze damu
Uvivu usiningie, bali niishike hamu
Ndoto zangu zitimie, matunda yawe matamu
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Uwe mwaka wa sururi, ‘sinitoke tabasamu
Na mengi yalo mazuri, yanifikie kwa zamu
Uwe mwaka wa fahari, nile vitamu vitamu
Ewe Mungu ujalie, uwe ni mwaka wa kheri
Rabbi Naomba baraka, Kwa wote wangu Umri
Nipe na nyingi fanaka, Niepushe na ya Shari
Niwe wa kuheshimika, Nifwate zako amri
Ewe Mungu ujalie, Uwe ni mwaka wa kheri
Mashaa Allah😍
❤❤❤