
MALENGA: KHALID SHARIFF
Bisimilahi ya mannani, kwa jina lako Karima,
Mola uso na kifani, natanguliza heshima,
Kisha kwa tumwa amini, na ahli zake kirama,
Maisha yangu jamani, bila Baba yaniuma.
Nimeketi na mamangu, ndiye baba ndiye mama
Si mwengine bali wangu, nimpendaye halima,
Kutimiza yalo yangu, mambo yake hujinyima,
Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.
Roho yangu huniuma, wengine kuita Baba,
Nimemzoea mama, sijui kuita baba,
Moyo wangu hunithoma, kama nlodungwa mwiba,
Maisha yangu jamani,bila baba huniuma.
Babangu sijamuona, tangu alipoondoka,
Hadi sasa Ni kijana, hajui nilipofika,
‘Menifanya Sina mana, mbeleni ‘tanikumbuka,
Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma,
Tena alosoma sana, ayua ovu na jema,
Na wala huruma hana, wana kumuachia mama,
Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.
‘metaabika mamangu, hakutaka kutuwata,
‘menilea na ndu’ zangu, Sharifa na farwata,
Na Mimi naapa Mungu, mamangu sitomuata,
Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.
Baba ndiye kiongozi, tena mwenye majukumu,
Sharifu hajamaizi, kwamba kwake ni muhimu,
Kutekeleza malezi, na tena kuwa na hamu,
Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.
‘Metufanya ni yatima, furaha kutukosesha,
Nikikumbuka ya nyuma, yalivyokuwa maisha,
Alivyoteseka mama, ili kutufurahisha,
Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.
Mashallah Farwa..really love mashairi yako..Allah akuzidishie ilmu uzidi tupa raha kwa mashairi yako
Shukran Sana😊😊
Aaaamiiiin